1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wakutana kukiwapo mivutano

Daniel Gakuba
26 Oktoba 2022

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amempokea kwa mazungumzo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, wakati nchi hizo zikitofautiana juu ya masuala kadhaa muhimu, yakiwemo mkakati wa umoja huo juu ya ulinzi na sera za uchumi.

https://p.dw.com/p/4IieR
Frankreich | Emmanuel Macron und Olaf Scholz
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani na Rais Emmanuel Macron Ufaransa wakiwa mjini ParisPicha: Sarah Meyssonnier /REUTERS

Rais Macron na Kansela Scholz wameshiriki mazungumzo hayo kwenye hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa katika katika ikulu ya Elsee mjini Paris, ambapo miongoni mwa masuala mengine wamejadili hali ilivyo nchini Ukraine.

Soma zaidi: Mvutano wa Ujerumani na Ufaransa wahujumu hatua za EU

Msemaji wa serikali ya Ufaransa, Olivier Veran amesema ziara ya Kansela Scholz inaonyesha uwezo wa nchi mbili, Ufaransa na Ujerumani kuzikabili tofauti baina yao pale maslahi ya nchi moja yanapogongana na ya nchi nyingine.

''Ziara ya Kansela wa Ujerumani kukutana na rais wa Ufaransa ni ushahidi wa urafiki ulio hai kabisa, na dhamira yetu ya kusonga mbele pamoja, na wakati mwingine kuvivuka vizuizi,''  amesema Veran na kuongeza kuwa nguvu ya uhusiano baina ya Ufaransa na Ujerumani iko katika kukubaliana kila wakati kuuinua Umoja wa Ulaya.

Deutschland Frankreich PK Ministerrat | Merkel und Macron
Ufaransa na Ujerumani zinao utaratibu wa vikao vya pamoja vya mawaziri, angalau mara moja kila mwakaPicha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

Kikao cha pamoja cha mawaziri chaahirishwa

Mipango ya awali ilihusisha pia kikao cha pamoja cha mabaraza ya mawaziri ya Ufaransa na Ujerumani, lakini hicho kiliahirishwa hadi Januari. Serikali za nchi hizo zimesema yapo mambo yanayojadiliwa kwanza kabla ya kupata muafaka juu ya masuala yanayohusu pande mbili.

Soma zaidi: Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Italia waizuru Ukraine

Tofauti kati ya Ujerumani na Ufaransa sio kitu kipya. Nchi hizo zenye uchumi mkubwa zaidi katika Umoja wa Ulaya na zinazotazamwa kama injini ya umoja huo, zimezoea kuwa na mitazamo inayokinzana juu ya usalama, nishati na masuala mengine.

Akizungumza mjini Brussels wiki iliyopita, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema lengo lake mara zote limekuwa kuimarisha umoja wa Ulaya na mahusiano mema na Ujerumani, na kuongeza kuwa kujitenga kando kwa Ujerumani hakuna tija kwa nchi hiyo wala kwa Ulaya kwa ujumla.

G8 Außenminister in Paris
Ujerumani na Ufaransa huchukuliwa kama injini inayouendesha Umoja wa UlayaPicha: AP

Scholz asema anawasiliana mara kwa mara na Macron

Alipoulizwa Ijumaa iliyopita ikiwa kuna mvutano baina ya nchi yake na Ufaransa, Kansela Scholz alijibu tu kuwa uhusiano baina ya nchi hiyo ni imara, na kuongeza kuwa huwa anafanya mazungumzo ya mara kwa mara na Rais Emmanuel Macron.

Soma zaidi: Putin awaonya Scholz na Macron dhidi ya kuipa silaha Ukraine

Vikao vya pamoja vya mawaziri wa Ufaransa na Ujerumani kwa kawaida hufanyika angalau mara moja kila mwaka, na cha mwisho kilifanyika kwa njia ya vidio mwezi Mei mwaka jana.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit alisema kuwa bado yapo mambo ambayo yanauzonga kila upande, na hakuna uhakika kama nchi hizo mbili zina mitazamo sawia juu ya baadhi ya mambo ya kimsingi.

 

Vyanzo: ape, dpae