1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vyalegezwa zaidi Ujerumani

Yusra Buwayhid
6 Mei 2020

Majimbo ya Ujerumani yamepewa uhuru wa kulegeza vikwazo vya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona, kwa sharti kwamba watashughulikia kwa haraka maambukizi mapya yatakayojitokeza.

https://p.dw.com/p/3brap
Deutschland Berlin Pressekonferenz Coronavirus | Angela Merkel
Picha: Reuters/M. Sohn

Hayo yameripotiwa baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya njia ya simu kati ya Kansela Angela Merkel na mawaziri wakuu wa majimbo ya Ujerumani. Aidha chini ya makubaliano hayo, serikali za majimbo zitalazimika kurejesha tena vikwazo vya kuzuia kueneo kwa maambukizi pale visa vipya vitakapojitokeza. Kwa namna hiyo, pindi wilaya au mji utakaporekodi zaidi ya maambukizi 50 kati ya wakazi 100,000 katika kipindi cha wiki moja, jimbo hilo litalazimika kurejesha tena hatua kali za kuchukua tahadhari.

Miongozo mingine ya serikali iliyojadiliwa hii leo, inasafisha njia ya kufunguliwa tena sehemu kubwa za umma Ujerumani, ikiwa ni wiki mbili tangu duru ya kwanza ya kulegezwa vikwazo kutangazwa nchini humo.

Serikali ya shirikisho la Ujerumani pamoja na serikali za majimbo zimekubaliana kuongeza muda wa kuendelea kutekelezwa sheria ya kuweka umbali wa mita moja na nusu kutoka mtu mmoja hadi mwengine hadi ifikapo Juni 5, lakini vyanzo kadhaa kutoka katika mazungumzo hayo vimesema msisitizo wa sheria hiyo umelegezwa.

Soma zaidi: Ujerumani kujadili kupunguza vikwazo vya virusi vya corona

Ujerumani ilikuwa imepiga marufuku watu zaidi ya wawili kukutana hadharani, pamoja na kila mmoja kutakiwa kuweka umbali wa mita moja na nusu kutoka kwa mwenzake. Lakini kuanzia sasa, familia mbili kutoka nyumba tofauti zitaruhusiwa kukutana, huku wakiendelea kuweka umbali huo unaotakiwa.

Deutschland Bund-Länder-Konferenz im Video-Chat
Mkutano wa shirikisho la serikali ya Ujerumani kupitia nji ya videoPicha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Majimbo yaanza kulegeza vikwazo

Baadhi ya majimbo yameshaanza kulegeza vikwazo hivyo. Katika jimbo la Saxony-Anhalt, wakazi wameanza kuruhusiwa kukutana kwa makundi ya watu hadi watano na katika jimbo la Bavaria jamaa wa karibu katika familia wanaruhusiwa kutembeleana.

Kadhalika Merkel na wakuu hao wa majimbo wamejadili suala la kuwaruhusu wanafunzi wote kurudi shuleni mwanzoni mwa mwezi Juni ambacho kawaida ni kipindi cha likizo ya shule ya majira ya joto. Wakati huo huo, maduka yote ya rejareja yameruhusiwa kufunguliwa tena.

Kwa upande wa michezo shirika la habari la dpa, limepokea taarifa kwamba Ligi Kuu ya Kandanda Ujerumani Bundesliga pamoja na ligi ya daraja la pili zimeruhusiwa tena kucheza mechi kuanzia katikati ya mwezi huu wa Mei lakini bila ya watazamaji.

Soma zaidi: Siku 100 tangu kisa COVID-19 kuthibitishwa Ujerumani

Wakosoaji wanasema serikali za majimbo zinaweza kupunguza juhudi za kufanyia wananchi vipimo vya virusi vya corona, kwa hofu kwamba idadi kubwa ya maambukizi ikirekodiwa watalazimika kurejesha tena vikwanzo kama vile watu kutakiwa kubakia majumbani.

Vyanzo: (dpa, rtre)