1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhalifuUjerumani

Ujerumani: Watu watatu wauawa katika shambulizi la kisu

24 Agosti 2024

Watu watatu wameuawa na wanne wamejeruhiwa vibaya katika shambulizi la kisu lililotokea katika tamasha la mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Solingen Ijumaa usiku. Polisi imeanzisha operesheni ya kumsaka mshukiwa.

https://p.dw.com/p/4js3p
Solingen, Ujerumani | Watu wauawa katika shambulizi la kisu
Polisi wameanzisha uchunguzi kuhusu shambulizi la kisu katika tamasha la mji wa SolingenPicha: Thilo Schmuelgen/REUTERS

Msemaji wa polisi ya mji ulio karibu wa Düsseldorf amesema polisi imeanzisha operesheni kubwa ya kumsaka mshukiwa, ambaye alifanikiwa kutoweka katika vurugu zilizofuatia. Mshambuliaji huyo aliwashambulia watu kiholela akitumia kisu. Tamasha hilo lilikuwa sehemu ya mfululizo wa matukio ya kusherehekea miaka 650 ya kuanzishwa mji huo.

Katika taarifa iliyochapishwa mtandaoni, meya wa Solingen Tim-Oliver Kurzbach amesema mji mzima upo katika mshtuko mkubwa na unaomboleza. Solingen ni mji wa wakaazi 160,000 unaopatikana umbali sawa kutoka Düsseldorf na Cologne.

Watu walikusanyika mjini humo jana jioni katika siku ya kwanza ya tamasha la siku tatu la kusherehekea kuasisiwa kwake. Zaidi ya wageni 75,000 walitarajiwa kuhudhuria sherehe hizo za siku tatu. Kufuatia shambulizi hilo, mji wa Solingen umezifuta kabisa sherehe hizo.