1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuruhusu tena mikusanyiko ya ibada

Yusra Buwayhid
1 Mei 2020

Wajerumani wataruhusiwa tena kukutana kwa ibada, kupeleka watoto wao kwenye bustani za mapumziko pamoja na kutembelea majengo ya makumbusho. Marufuku ya hafla za mikusanyiko mikubwa ya watu itaendelea kuwepo.

https://p.dw.com/p/3bdtk
BG Deutschland Corona Lockerung
Picha: Getty Images/S. Gallup

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pamoja na wakuu wa majimbo 16 nchini humo wamekubaliana kupunguza zaidi vikwazo vilivyokuwa vimewekwa kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Kulingana na Kansela Merkel, viwanja vya michezo vya watoto, majengo ya makumbusho, pamoja a bustani za maua na wanyama zitafunguliwa tena lakini kwa masharti maalumu. Ameongeza kwamba hatua nyingine zitatangazwa ifikapo Mei 6. Aidha Merkel ameonya kwamba Ujerumani lazima ijitahidi kushusha zaidi idadi ya maambukizi mapya ya kila siku na kwamba sheria ya kuweka umbali kutoka mtu mmoja hadi mwingine lazima izingatiwe katika maeneo ya umma ili kuzuia kuongezeka kwa maambukizo.

Aidha maeneo ya ibada kama vile makanisa na miskiti pia itafunguliwa tena. Hafla zingine za kidini, ikiwa ni pamoja na harusi, kubatizwa na mazishi pia zinaruhusiwa. Majimbo yote ya nchini Ujerumani yatalazimika kuhakikisha tahadhari za kujikinga na maambukizi hayo zinatekelezwa. Mikusanyiko ya kidini tayari imesharuhusiwa katika majimbo ya Saxony na Thuringia nchini humo.

Mikahawa haitofunguliwa

Merkel amesema kufungua mikahawa wakati huu itakuwa shida kwa sababu, ni vigumu kujua iwapo watu waliokaa meza moja ni kutoka familia moja, au kutoka familia tofauti.

Aidha Kansela huyo amesema maamuzi waliyoyafanya Alhamisi ni hatua za awali, na kwamba hatua zingine zitatangazwa wiki ijayo.

Sheria za kuweka umbali wa takriban mita moja na nusu kutoka mtu mmoja hadi mwengine itabakia kuwepo hadi Mei 10, ambapo Merkel na viongozi wote wa majimbo watakapokutana kuamua zaidi Jumatano ijayo.

Deutschland Berlin Pressekonferenz  Coronavirus | Angela Merkel
Kansela Angela Merkel akiwa katika mkutano na waandishi haari - 30.04.2020Picha: Getty Images/S. Gallup

Hatua hazihatarishi maisha ya raia

Profesa Karl Lauterbach mtaalamu wa udhibiti wa magonjwa ameiambia DW kwamba mabadiliko yaliyotangazwa jana hayatohatarisha maisha ya raia.

Alipoulizwa iawapo Wajerumani wataruhusiwa kusafiri hivi karibuni, Merkel alijibu kwamba suala la safari za kwenda mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya bado halikuwekwa kwenye ajenda ya mazungumzo. Seriklai ya Merkel awali iliongeza muda wa onyo dhidi ya safari za kimataifa hadi Juni 14.

Naye Waziri wa Fedha wa Ujerumani Olaf Scholz ameonya kwamba nchi inahitajika kuchukua maamuzi mzuri sio kupoteza mafanikio iliyoyapata katika kupunguza kuenea kwa virusi vya corona.

Vyanzo: rtre/dw