1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJapan

Shigeru Ishiba atangazwa kuwa waziri mkuu mpya wa Japan

Sylvia Mwehozi
27 Septemba 2024

Waziri wa zamani wa ulinzi wa Japan Shigeru Ishiba atakuwa waziri mkuu wa Japan wiki ijayo baada ya kushinda kura ya uongozi wa chama tawala cha kihafidhina siku ya Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4lAcK
Japan Shigeru Ishiba-waziri mkuu mteule
Japan Shigeru Ishiba-waziri mkuu mteulePicha: Kim Kyung-Hoon/REUTERS

Japan imepata waziri mkuu mpya leo baada ya chama tawala cha Liberal Democratic, LDP, kumchagua waziri wa zamani wa ulinzi Shigeru Ishiba kuwa kiongozi wake kumrithi Fumio Kishida aliyetangaza mwezi Agosti kutowania tena nafasi hiyo.

Ishiba mwenye umri wa miaka 67 amechaguliwa kwa kura 215 dhidi ya 194za mwanasiasa anayeegemea sera za kizalendo, Sanae Takaichi, ambaye iwapo angechaguliwa angekuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza taifa hilo.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi kwenye mkutano wa chama chake ulifanyika mjini Tokyo, Ishiba ameahidi kufanya kazi kwa ujasiri mkubwa na kuifanya Japan kuwa nchi salama kwa kila raia wake.

Salamu za pongezi zimeanza kumiminika kutoka kila pembe ya dunia huku mataifa hasimu mfano wa China imesema inalenga kufanya kazi na Ishiba kuimarisha mahusiano yaliyopwaya kati ya Tokyo na Beijing.

Ishiba aliwahi kukaribia kuwa waziri mkuu mwaka wa 2012 aliposhindwa na Shinzo Abe, kiongozi wa muda mrefu zaidi wa Japan ambaye aliuawa baadaye.

Japan Shigeru Ishiba-waziri mkuu mteule
Japan Shigeru Ishiba -waziri mkuu mteulePicha: Kim Kyung-Hoon/REUTERS

Chama cha LDP kimetawala Japan kwa miongo kadhaa na kina wabunge wengi, ikimaanisha kwamba Ishiba atachaguliwa kuwa waziri mkuu na bunge siku ya Jumanne.Japan, Korea Kusini na Marekani kuimarisha ushirikiano wao

Kama waziri mkuu, Ishiba atahitaji kukabiliana na vitisho vya usalama vya kikanda, kutoka kwa China inayozidi kuwa na msimamo na uhusiano wake na Urusi hadi majaribio ya makombora yaliyopigwa marufuku ya Korea Kaskazini.

Msukumo wake wa kuboresha jeshi na kutoa wito wa kuundwa kwa NATO ya Asia unaweza kuikasirisha Beijing, lakini amekuwa makini na matamshi yake kuhusu China.Chama tawala nchini Japan kumchagua kiongozi mpya atakayekuwa pia Waziri Mkuu

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China alisema nchi hiyo inataka kuboresha uhusiano na Japan, kwa sababu ya "maendeleo endelevu, thabiti na uhusiano kati ya China na Japan unatimiza maslahi ya kimsingi ya nchi hizo mbili."