Senegal kupiga kura leo
26 Februari 2012Koloni hilo la zamani la Ufaransa ni moja kati ya nchi ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuanzisha demokrasia katika bara la Afrika, ikijivunia chaguzi mbali mbali bila kizuwizi tangu kupata uhuru mwaka 1960. Ni taifa pekee katika eneo la Afrika magharibi ambayo haijakumbwa na mapinduzi ya kijeshi.
Hata hivyo juhudi za rais Wade za kuwania kipindi cha tatu cha utawala kinaonekana kuwa mtihani mgumu kwa sifa ya kidemokrasia ya Senegal , na kusababisha wasi wasi wa kimataifa baada ya wiki kadha za maandamano ambayo yamesababisha watu sita kuuwawa.
Takriban watu milioni 5.3 wamejiandikisha kupiga kura hii leo.
Wade anakabiliwa na wagombea 13 wa kiti cha urais ikiwa ni pamoja na mawaziri wakuu watatu wa zamani , Idrissa Seck, Macky Sall , Moustapha Niasse na kiongozi wa chama cha kisoshalist Ousmane Tanor Dieng. Hakuna ambaye amejitokeza kuwa na nafasi ya mbele dhidi ya Wade.
licha ya kutumikia vipindi viwili madarakani, muda ambao aliuanzisha binafsi, Wade amesema mabadiliko ya katiba ya mwaka 2008 yanayorefusha kipindi cha uongozi hadi miaka saba yanamruhusu kutumikia vipindi vingine viwili.
Kiongozi mkongwe Afrika
Akiwa kiongozi wa pili katika bara la Afrika mwenye umri mkubwa baada ya kiongozi wa Zimbabwe Robert Gabriel Mugabe mwenye umri wa miaka 88, Wade amesema anahitaji muda zaidi kumaliza mradi wake mkubwa . Lakini ameshutumiwa kwa kutaka kumuweka mtoto wake wa kiume Karim Wade kama mrithi wake.
Ujumbe wa ngazi ya juu wa amani kutoka umoja wa Afrika ukiongozwa na rais wa zamani wa nigeria Olusegun Obasanjo umependekeza kuwa iwapo Wade atashinda , atastaafu baada ya miaka miwili.
Si Wade wala upande wa upinzani ambao umekubali mapendekezo hayo.
Kundi la Juni 23
Kundi linalojulikana kama vuguvugu la Juni 23, ambalo ni muungano wa vyama vya upinzani na wanaharakati , limetoa wito siku ya Jumamosi kwa uchaguzi wa rais kutayarishwa katika muda wa miezi sita hadi tisa , ambapo Wade hatashiriki. Kampeni ya kumpinga Wade ilifanywa na kundi la wanamuziki wa rap, wagombea wa kiti cha urais, wanaharakati na mwanamuziki maarufu ambaye amepata tuzo ya Grammy ya muziki Yousou N'Dour, ambaye amezuiwa na mahakama kugombea kiti cha urais.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Bruce Amani