Rais wa Ukraine akataa kuurefusha muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano
1 Julai 2014Rais Petro Poroshenko ambaye anaishutumu Urusi kwa kuuchochea mzozo huo wa mashariki mwa Ukraine amepuuzilia mbali juhudi za Urusi za kuutuliza mzozo huo na kuwashutumu waasi hao wanaoungwa mkono na Urusi kwa kushindwa kuyaheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano au kuuzingatia mpango wake wa kutafuta amani.
Katika hotuba aliyoitoa kwa taifa hapo jana usiku,Poroshenko ameapa kukabiliana na waasi hao ili kuiokoa Ukraine kutoka mikononi mwa waasi na kuongeza kuwa uamuzi wa kutorefusha makubaliano ya kusitisha mapigano ni ujumbe kwa magaidi na wanamgambo kuwa watakabiliwa ipasavyo.
Majeshi ya Ukraine yanaripotiwa hii leo kuanzisha mashambulizi dhidi ya waasi hao mashariki mwa Ukraine licha ya juhudi za dakika za mwisho mwisho za viongozi wa Ulaya hapo jana kutafuta kuuongeza muda wa kusitisha mapigano.
Mapigano yazuka upya mashariki mwa Ukraine
Spika wa bunge la Ukraine Oleksandr Turchynov ameliambia bunge hii leo kuwa awamu nyingine ya opresheni za kijeshi imerejea katika ngome za waasi hao.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande,Kansela wa Ujerumani Angela Merkel,Rais wa Urusi Vladimir Putin na Poroshenko jana walifanya mazungumzo ya pande nne kwa siku ya tano mfululizo kutafuta njia muafaka ya angalau kuupunguza mzozo huo wa Ukraine.
Lakini licha ya juhudi hizo za kidiplomasia, mapigano yameripotiwa leo katika eneo hilo la mashariki.Raia wanne wameuawa katika mashambulizi ya asubuhi ambayo pia yamewajeruhi watu wengine watano na kufikisha idadi ya waliouawa katika mzozo huo tangu uanze kufika 450
Viongozi wa Ulaya watazidisha juhudi za kidiplomasia
Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius amesema Ufaransa na Ujerumani hazitalegeza kamba katika juhudi za kutafuta amani nchini Ukraine na kuongeza kuwa kile wanachotafuta hivi sasa ni suluhu la muda mrefu la kusitisha mapigano,Ukraine kuwa na nguvu za kulinda mipaka yake na pia suala la kuhakikisha waliotekwa nyara wanaachiwa huru.
Urusi kwa upande wake imesema uamuzi wa Poroshenko wa kutorefusha muda wa makubaliano ya kusitisha mapigano umetokana na shinikizo kutoka nje na kwamba imesikitishwa na uamuzi huo huku ikizitaka nchi za kigeni kukoma kuitumia Ukraine kama chambo cha kufanya siasa za udhibiti wa kanda.
Mbunge wa Ujerumani Nobert Roettgen ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu masuala ya kigeni amekiambia kituo cha redio cha Ujerumani kuwa Umoja wa Ulaya leo unatarajiwa kufanya uamuzi wa kuiwekea Urusi vikwazo zaidi kwa kuendelea kuuchochea mzozo wa mashariki mwa Ukraine.
Mwandishi:Caro Robi/Reuters/afp/ap
Mhariri:Yusuf Saumu