1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ongezeko la visa vya dhulma za kijinsia Marsabit Kenya

Michael Kwena12 Januari 2023

Matukio ya dhulma za kijinsia yameripotiwa kuongezeka maradufu jimboni Marsabit nchini Kenya wakati maelfu ya wafugaji wakiendelea kuathirika na makali ya ukame.

https://p.dw.com/p/4M3DI
Wahanga wa dhulma hizo hawafike mahakamani
Wahanga wa dhulma hizo hawafike mahakamaniPicha: Simon Maina/AFP

Makali ya kiangazi yameendelea kuwa changamoto katika familia nyingi za wafugaji hapa Marsabit na kuchangia mizozo ya kifamilia kuongezeka zaidi.

Hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa matukio ya dhulma za kijinsia majumbani kwani wanandoa wengi hawana uwezo wa kuzikimu familia zao kwa wakati huu.

Kulingana na mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la MWADO Nurria Golloh,visa vya dhulma za kujinsia vimeongezeka kutokana na matatizo ya afya ya kiakili kwa wafugaji waliowapoteza mifugo yao kutokana na makali ya ukame wa muda mrefu unaoshuhudiwa hapa Marsabit.

''Kesi za dhulma zimeongezeka kabisa''

Bi Nurria Pamoja na wadau wengine,sasa wameanzisha harakati za kuwafikia wafugaji kwa ushauri nasaha kama sehemu ya kupunguza visa hivyo ambavyo zimeendelea kuongezeka hapa Marsabit

"Tangu wakati wa janga la COVID 19 na ikafuatiwa na ukame wa muda mrefu,kesi za dhulma zimeongezeka kabisa.Familia nyingi zimesambaratika kwa sababu watu wamepoteza mifugo yao.”

Mabadiliko ya tabia nchi

Kwa misimu minne mtawalia mvua imekosa kunyesha jimboni Marsabit
Kwa misimu minne mtawalia mvua imekosa kunyesha jimboni MarsabitPicha: Michael Kwena/DW

Akizungumza pembezoni mwa mkutano huo,afisa mkuu mtendaji wa shirika la kijamii la CIFA Salad Liban ameeleza kwamba,nyingi za visa vya dhulma za kijinsia zimekosa kuripotiwa katika idara ya polisi akifafanua kuwa,wafugaji wengi hawapendi maswala ya kuelekea mahakamani kutafuta haki.

Afisa huyo amehusisha ongezeko la dhulma za kijinsia na ufukara uliosababishwa na kiangazi kilichowauwa mifugo hapa Marsabit.

"Kuna ongezeko la dhulma za kijinsia kwa sababu watu walikuwa na mifugo na waliwapoteza.mama akiitisha pesa,mzozo unaibuka.”

Kwa misimu minne mtawalia,mvua imekosa kunyesha jimboni hapa huku maelfu ya mifugo wakiangamia na hali hiyo imeendelea kuwaathiri wafugaji kiakili na kusababisha mizozo majumbani.

Marsabit ni miongoni mwa majimbo ishirini na tatu zilizoorodheshwa kuwa katika hali mbaya ya ukame wakati huu.