1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaNiger

Niger yazindua kampeni ya chanjo dhidi ya Malaria

21 Septemba 2024

Niger imekuwa nchi ya hivi karibuni katika kanda ya Afrika Magharibi kuzindua mpango wa chanjo ya Malaria ili kujaribu kuzuia ugonjwa huo hatari.

https://p.dw.com/p/4kvBd
Kamerun Datcheka | Impfkampagne gegen Malaria
Muuguzi akijiandaa kutoa chanjo ya malaria kwa mtoto mchanga katika kituo cha afya cha Datcheka, Cameroon.Picha: Desire Danga Essigue/REUTERS

Waziri wa afya Garba Hakimi amesema wamezindua kampeni kubwa ya chanjo huku awamu ya kwanza ikifanyika Alhamisi katika mji wa Kusini Magharibi wa Gaya, kitovu cha ugonjwa wa malaria unaoenezwa na mbu.

Kwa wastani wagonjwa wa malaria milioni tano hurekodiwa nchini Niger kila mwaka huku zaidi ya watu 5,000 wakipoteza maisha.

Soma pia: Dola bilioni moja zaahidiwa kuwezesha uzalishaji wa chanjo Afrika

Kulingana na takwimu za shirika la afya duniani WHO, mnamo mwaka 2022, malaria ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 600,000 duniani kote – asilimia 95 kati yao wakiwa barani Afrika na asilimia 80 wakiwa Watoto chini ya umri wa miaka mitano.

WHO imesema katika taarifa kuwa dawa ya kupambana na malaria RTS,S – iliyotengenezwa na kampuni ya dawa ya Uingereza ya GSK – itatumika kwenye kampeni hiyo ya chanjo nchini Niger ambayo iliidhinisha mwaka 2022.