"Msichana wa Kitunisia" Blogu iliyopata DW BOBs Award 2011
13 Aprili 2011Blogu iliopewa jina la "A Tunisian Girl" (Msichana wa Kitunisia) imeshinda tuzo ya blogu ya kimataifa ya THE BOBs inayotolewa na Deutsche Welle-BOB. Tuzo hiyo ilitolewa Aprili 12 mjini Bonn kwa kupitia anuani ya internet http://atunisiangirl.blogspot.com.
Lina Ben Mhenni mwenye umri wa miaka 27 ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Tunis. Blogu yake hiyo ilihusika pia na ukandamizaji na uchujaji wa habari wakati wa utawala wa rais wa zamani Zein el-Abidinne Ben Ali.
Blogu yake ikatoa mchango wakati wa vuguvugu la upinzani Desemba 2010 na Januari 2011 katika mji wa Sidi Bouzid na Kasserine na kuripoti kuhusu ukandamizaji wa vyombo vya dola na machafuko. Tangu wakati huo Mhenni anaandika juu ya matatizo yanayoikabili Tunisia kuelekea Demokarasia. Kwa muda mrefu blogu yake ilipigwa marufuku nchini Tunisia, na ikiwezekana tu kusoma yaliomo ikiwa uko nje ya nchi hiyo.
Kutokana na uteuzi huo wiki hii na jopo la kimataifa, tuzo hiyo itatolewa katika fani sita tofauti wakati wa kongamano la Deutsche Welle la vyombo vya habari duniani tarehe 20 Juni mwaka huu 2011 mjini Bonn.