Mkutano wa kilele kuhusu wakimbizi barani Ulaya
28 Agosti 2017Gazeti la Stuttgarter Nachrichten, kuhusiana na mkutano wa kilele wa mataifa manne kujadili sera kuhusu wakimbizi barani Ulaya limeandika.
"Katika suala hili la sera za wakimbizi, matarajio ya wananchi ni makubwa lakini kwa upande wa serikali hali ni ngumu. Kwa hiyo itavunja moyo , kwa atakayezungumzia kupiga hatua zaidi kuunga mkono matamshi ya kansela katika mkutano huo utakaohudhuriwa na viongozi wa Ufaransa, Italia na Uhispania ambapo watajumuika na kujadili pamoja na viongozi wa mataifa jirani ya Ulaya kutoka Afrika kaskazini. Kwa kiasi kikubwa ndio yanahusika na taizo hilo."
Gazeti la Badische Zeitung nalo linazungumzia kuhusu mkutano huo , mhariri anandika ...
"Bila shaka kungekuwa na wahamiaji haramu wachache , iwapo bara la Afrika halingekuwa na umasikini, rushwa na kutoheshimu haki , na kusababisha watu kuhatarisha maisha yao kufanya safari ya hatari badala ya kubaki katika mataifa yao. Na ni kutokana na hali hiyo ya kutokuwa na hakika ya maisha yao ndio sababu wasafirishaji haramu wananufaika katika kazi yao hiyo. Kufikiria njia mbadala ya kuwasaidia watu hawa sio jambo la kijinga. Iwapo kutakuwa na watu wachache watakaofanyakazi hii ya kuwasaidia wahamiaji kufanya safari hizi , kutakuwa pia wakimbizi watakuwa wachache."
Kampeni za Uchaguzi Ujerumani
Kampeni za uchaguzi nchini Ujerumani zinaingia katika hatua ya kuvutia zaidi. Gazeti la Rheinpfalz , la mji wa Ludwigshafen linazungumzia kuhusu marufuku ya ushirikiano katika nyanja ya elimu ..
"Kuondolewa kwa marufuku ya ushirikiano, majimbo ya Ujeruimani yatapoteza kitu muhimu cha utambulisho wao. Itakuwa ujinga kufikiri , kwamba serikali kuu itoe malipo, na serikali za majimbo zitimize zinayotakiwa kutimiza. Hata katika maeneo mengine serikali za majimbo zimo katika mbinyo, uwezo wake umo hatarini."
Kuhusu mada hiyo hiyo ya kampeni gazeti la Neue Osnabrücker Zeitung linaandika kuhusu kashfa ya dizeli. Mhariri anaandika kwamba mwanzo mpambano katika kampeni ulionekana kutokuwa na mvuto, lakini sasa hali inaanza kuwa moto moto, ikihusisha malumbano ya kashfa ya dizeli. Hakuna mada ambayo ina ncha nyingi na kuleta hamasa kwa wananchi kama hii, na katika ujumla wake wanasiasa wote wamo. Wanapaswa kulumbana kama anavyofanya Host Seehofer wa chama cha CSU na Cem Özdemir wa chama cha kijani. Tunasubiri bado, hata hivyo mhariri anaandika, kuona iwapo matamshi ya nani yanaweza kuzua malumbano makubwa zaidi.
Trump na wanazi mamboleo
Gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung , linaandika kuhusu msamaha aliotoa rais Donald Trump kwa sheriff Joe Arpaio, licha ya kuhusishwa na kashfa kadhaa za kibaguzi. Mhariri anaandika.
"Jela ya muda iliyojengwa kwa mahema ambayo imetayarishwa na kiongozi wa eneo kwa Marekani akijulikana kama Sheriff , Joe Arpaio katika jangwa la Arizona pamoja na udhalilishaji aliotayarisha dhidi ya jamii ya watu wachache nchini humo, ni suala lililoshutumiwa kwa kiasi kikubwa nchini Marekani, na pia upinzani alioonesha seneta kutoka chama cha Republican John McCain dhidi ya msamaha uliotolewa na rais Trump kwa kiongozi huyo. Kwa hatua ya rais Trump kumpa msahama kiongozi huyo, amewapa nguvu wale wenye siasa kali za mrengo wa kulia. Trump amechukua hatua hiyo licha ya kesi inayomkabili Arpaio mahakamani, na hii inaonesha jinsi Trump asivyouheshimu mfumo wa sheria nchini humo."
Hayo ndio baadhi ya maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani kwa leo (28.08.2017).
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman