1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aonya juu ya kuongezeka maambukizo ya korona

28 Agosti 2020

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameonya kwamba janga la virusi vya korona linaweza kuwa baya zaidi katika miezi ijayo na hivyo maisha hayatarudi kwenye hali ya kawaida hadi chanjo itakapopatikana.

https://p.dw.com/p/3heHd
Sommer-PK mit Bundeskanzlerin Merkel
Picha: AFP/Pool/M. Kappeler

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin, Kansela Merkel alisema Ujerumani bado ina miezi michache ya mwisho migumu kwa mwaka huu, akionya kwamba huenda majira ya mapukutiko na kipupwe yakawapa Wajerumani changamoto mpya ya janga la virusi vya korona. 

"Lazima tujuwe kuwa mambo yatakuwa magumu zaidi kwa miezi ijayo kulinganisha na kipindi hiki cha kiangazi. Kwenye kiangazi, tumefurahikia uhuru na ulinzi kwa miale ya jua tukiwa nje. Miezi ijayo tutakuwa na jukumu la kushusha idadi ya maambukizo tukiwa ndani, kazini, skuli na majumbani mwetu," alisema Merkel.

Onyo la Merkel linatokana na utafiti wa kitaalamu unaoonesha kuwa virusi vya korona vinaweza kusambaa kwa haraka zaidi pale watu wanapojifungia kwenye eneo dogo kuliko pale wanapokuwa kwenye maeneo mapana ya wazi.

Ujumbe huu wa hadhari unakuja wakati huu ambapo tayari idadi ya maambukizo imepanda kwa kiwango kikubwa ndani ya wiki chache zilizopita. Leo hii idadi ya waliosajiliwa kuambukizwa wamefikia 1,500 - ikiwa ni siku ya pili mfululizo.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Robert Koch, watu waliokwishaambukizwa tangu janga hili lianze nchini Ujerumani imefikia 239,507, ambapo 9,288 kati yao wameshapoteza maisha. 

Huenda Ulaya ikachukuwa hatua dhidi ya Urusi

Russland Moskau | Alexej Nawalny, Oppositionspolitiker
Kiongozi wa upinzani wa Urusi, Alexei Navalny.Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Golovkin

Katika hatua nyengine, Kansela Merkel hakuondosha uwezekano wa Ulaya kuchukuwa hatua ya pamoja kujibu tuhuma za kulishwa sumu kwa kiongozi wa upinzani wa Urusi, Alexei Navalny, ambaye kwa sasa anatibiwa katika hospitali ya Charite mjini Berlin.

Merkel alisema anaamini ni wajibu wa Ujerumani kufanya kila kitu kusahihisha kilichotokea. "Ilikuwa sahihi na vyema kwamba Ujerumani ilisema iko tayari kumchukuwa Bwana Navalny na nawashukuru madaktari wa Hospitali ya Charite."

"Sasa tutafanya kila tuwezalo kulisahihisha. Na baada ya kuwa na usahihi wa mazingira haya, kama tulivyofanya kwa kadhia ya Bwana Skripal, tutajaribu pia kuwa na hatua ya pamoja ya Ulaya na sio kama nchi moja moja."

Katika mkasa wa jasusi Sergei Skripal aliyepewa sumu nchini Uingereza, takribani mataifa 30 ya Magharibi yaliwafukuza wanadiplomasia wa Urusi.