Libya kungali moto
18 Julai 2011Vikosi vya waasi vimesema kuwa vimefanikiwa kuingia mji huo lakini bado haukutiwa mikononi mwao. Mji wa Brega, unadhibitiwa na majeshi ya Gaddafi, tangu mwezi wa Aprili.
Ripoti zinasema, kiasi ya waasi 13 wa Libya wameuawa na takriban 200 wamejeruhiwa, tangu mapigano ya kuudhibiti mji wa bandari Brega, kuanza siku ya Alkhamisi.
Wakati huo huo, upande wa magharibi waasi walifanikiwa kuvisukuma nyuma vikosi vya Muammar Gaddafi. Na hii leo, televisheni ya Libya pia imeripoti kuwa wilaya ya Tajoura, mashariki ya mji mkuu wa Libya, imeshambuliwa na ndege za jumuiya ya kujihami ya NATO.
Hayo ni mashambulio ya kwanza kufanywa na NATO, karibu na mji mkuu baada ya siku kadhaa. Ripoti hiyo imesema kuwa mashambulio hayo yalilenga vituo vya kiraia na kijeshi, lakini haikueleza zaidi kuhusu vituo hivyo wala haikutaja kama kulikuwepo majeruhi.