'Laana ya rasilimali za Congo'
Madini ya Kobalti na Koltani yanapatikana kwa wingi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Lakini, kutokana na msukosuko wa kikanda, madini hayo huwavutia wapiganaji, unyanyasaji na machafuko
Utajiri wa rasilimali na fursa za machafuko
Katika mikoa tete ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, madini kama dhahabu na bati huyavutia makundi ya wapiganaji. Makundi hayo huwanyanyasa watu, wakiwemo watoto, kuchimba "madini ya maeneo ya migogoro'. Mapato hutumika kununua silaha ili kuyakamata maeneo zaidi na kuendeleza mapigano
Kuwalinda raia na operesheni halali za uchimbaji madini
MONUSCO, jeshi kubwa kabisa na la gharama kubwa la kulinda amani, linafanya kazi kuweka utulivu katika mikoa ya Kivu kaskazini na Kusini, ambayo ndio kitovu cha machafuko nchini humo. Vikosi vya usalama huweka doria katika vijiji vya uchimbaji madini kama Nzibora, kinachopatikana ukingoni mwa Zola Zola, chimbo halali la madini ya cassitérite
Kutengeneza simu za mkononi kwa gharama ya maisha ya binaadamu
Cassiterite ni moja tu ya madini yanayotumika katika simu za mkononi. Nusu ya madini hayo ulimwenguni inatoka Afrika ya Kati. Uuzaji wa bati, dhahabu na madini mengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umekuwa chini ya uchunguzi tangu 2010, wakati sheria zilipitishwa Marekani zikihitaji orodha ya kampuni za Kimarekani kuhakikisha mauzo yao sio madini ya kutoka katika maeneo ya migogoro
Kuthibitisha uhalli wa madini
Picha ya tangazo kijijini Nzibira inafafanua namna vifurushi vya madini vinahitaji kufungwa vizuri na kuwekwa kibandiko na mkaguzi wa mgodi ili chanzo cha madini hayo kithibitishwe na kampuni za Marekani. Mfumo huo, hata hivyo, una mapengo mengi. Migodi haramu inaweza kuuza kwa urahisi madini kwenye soko la magendo au kufanya biashara haramu na mgodi halali ili yawekwe katika vifurushi huko
Unyanyasaji wa watoto
Licha ya juhudi za makundi ya haki za binaadamu, ukiukaji wa haki za binaadamu bado umekithiri katika operesheni za uchimbaji madini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Watoto kama vile Esperance Furahaare, aliyetekwa nyara na kubakwa na wapiganaji wakati akiwa na umri wa miaka 14, ni waathiriwa wa unyanyasaji na machafuko.
Athari za Kimazingira
Migodi, ambayo ni changamoto kwa polisi, inaweza pia kuathiri mazingira na jamii zilizo karibu. Katika migodi haramu, maji taka yanayomwagika aghalabu huishia kwenye vyanzo vya maji ya wakaazi, na kuyachafua
Mustakabali usiojulikana wa sheria zinazokabili madini ya maeneo ya migogoro
Wabunge wa Marekani wanajaribu kuujadili mswada ambao utayafuta mageuzi ya mwaka wa 2010. Wwanahoji Sheria ya Dodd-Frank imezuia maendeleo ya kiuchumi Marekani na haijatatua unyanyasaji Afrika ya Kati. Huku kampuni za Marekani zikihitaji kuhakikisha zinanunua madini yasiyotoka maeneo ya migogoro, kile zinachohitajika kufanya ni kuwauliza wanaowauzia, sio ushahidi wa uuzaji au yalikotoka