Kutafuta habari kwenye Mtandao – Teknolojia mpya ya Habari
28 Aprili 2011Je wewe huwasiliana na jamaa zako nchini Marekani? Je umewahi kutoa maelezo yako mafupi kwenye mtandao wowote wa kijamii? Au je, hutumia mtandao wa Intaneti kufanya utafiti wa kazi zako?
Katika sehemu nyingi Barani Afrika, ukosefu au huduma duni na za pole pole za mtandao wa Intaneti bado ni kikwazo na tatizo kubwa kwa watumiaji wake. Lakini sasa bara hili limo mbioni kurekebisha hali hii.
Teknolojia mpya ya mawasiliano inakupa fursa nzuri ya kuboresha maisha yako kupitia huduma hizi na hasa kwa wanaotumia simu za mkononi ambazo zimerahisisha sana mawasiliano. Lakini teknolojia hii mpya pia inakuja na changamoto zake.
Na hii ndio sababu Noa Bongo inajaribu kulipigia mbizi suala hili ili kutoa mwangaza zaidi kuhusu matumizi ya teknolojia hii mpya. Kupitia mchezo wa redio, tunasikia hadithi kuhusu kundi la vijana wanaoamua kijitosa katika biashara ya kutoa huduma za teknolojia hii mpya ya mawasiliano. Sikiliza upate kufahamu masaibu yanayowakumba baada ya kuanzisha mkahawa wao wa kutoa huduma hizi za intaneti.