1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yashinda medali mbili za dhahabu London Marathon

21 Aprili 2024

Mwanariadha Alexander Munyao ameipa Kenya ushindi mwingine katika siku ambayo mashindano ya mbio za marathon za London yamemkumbuka bingwa wa mwaka jana Kelvin Kiptum.

https://p.dw.com/p/4f1sq
Mbio za London Marathon 2024 | Alexander Mutiso Munyao na Peres Jepchirchir
Washindi wa medali za dhahabu upande wa wanaume na wanawake kwenye mashindano ya London Marathon 2024. Kutoka kushoto ni Alexander Mutiso Munyao na Peres Jepchirchir, wote wawili ni raia wa Kenya.Picha: Justin Tallis/AFP/Getty Images

Mbio zilizoanza kwa sekunde thelathini za kupiga makofi kwa heshima ya Kiptum, aliyefariki Februari katika ajali ya gari, zilikamilika kwa Mkenya mwenzake na rafiki yake kumaliza katika nafasi ya kwanza.

Mutiso Munyao alitumia muda wa saa mbili, dakika nne na sekunde moja, huu ukiwa ushindi wake wa kwanza katika mashindano makubwa ya marathon.

Mutiso Munyao alisema alizungumza na Kiptum baada ya ushindi wake mjini London mwaka jana na kuwa mshika rikodi huyo wa dunia huwa akilini mwake anaposhiriki mashindano. Muethiopia Kenenisa Bekele mwenye umri wa miaka 41 alimaliza katika nafasi ya pili.

Kenya imeshinda pia medali ya dhahabu, baada ya bingwa wa Olimpiki Peres Jepchirchir alipomaliza wa kwanza katika mbio za wanawake na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea dhahabu yake katika Michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka huu.

Jepchirchir alimpiku mshikilizi wa rekodi ya dunia Muethiopia Tigst Assefa kwa kutumia muda wa saa mbili, dakika 16 na sekunde 16. Mkenya Joyciline Jekposgei alimaliza wa tatu.