1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Israel yashambulia Lebanon baada ya mauaji ya watu 492

24 Septemba 2024

Israel imetangaza mashambulizi mapya ya anga kwenye ngome za Hezbollah nchini Lebanon, siku moja baada ya watu 492, wakiwemo watoto 35, kuuawa katika mashambulizi mabaya zaidi ya mabomu tangu vita vikali vya mwaka 2006.

https://p.dw.com/p/4l0oT
Mifumo ya anga ya Israel
Mifumo ya anga ya IsraelPicha: Baz Ratner/AP/picture alliance

Israel imetangaza mashambulizi mapya ya anga kwenye ngome za Hezbollah nchini Lebanon hii leo, siku moja baada ya watu 492, wakiwemo watoto 35, kuuawakatika mashambulizi mabaya zaidi ya mabomu tangu vita vikali vya mwaka 2006.

Mashambulizi hayo ya usiku kucha ya Israeli yanakuja baada ya nchi hiyo kusema kuwa imeua idadi kubwa ya wanamgambo wakati iliposhambulia takriban shabaha 1,600 za kundi la Hezbollah kote nchini Lebanon.

Kwa upande wake, Hezbollah imesema leo kuwa imerusha makombora katika kambi za kijeshi za Israel saa chache baada ya makombora yake 180 na droni kuvuka anga ya Israel na kuwalazimu watu katika mji wa Haifa kukimbilia usalama wao.

Soma: Hezbollah, Israel zashambuliana vikali usiku wa kuamkia Jumapili

Viongozi wa dunia wameelezea wasiwasi kuhusu kasi ya mashambulizi hayo katika mstari wa mbele wa vita wa Lebanon .

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Lin Jian amesema "China inafuatilia kwa makini sana mvutano uliopo kati ya Lebanon na Israel, na inashtushwa sana na hatua husika za kijeshi ambazo zimesababisha vifo vingi."

Jian ameongeza kuwa China inapinga ukiukwaji wa uhuru na usalama wa Lebanon na pia inashtumu hatua zote zinazosababisha mateso kwa raia.