1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliouwawa Lebanon yazidi kuongezeka

Angela Mdungu
24 Septemba 2024

Idadi ya watu waliouwawa kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel Kusini mwa Beirut ndani ya siku mbili sasa ni zaidi ya watu 550. Miongoni mwa waliouwawa katika shambulio la Jumanne ni Kamanda wa kundi la Hezbollah.

https://p.dw.com/p/4l2ZD
Israel imeendelea kufanya mashambulizi Kusini mwa Lebanon
Moto ukifuka baada ya mashambuli ya Israel Kusini mwa LebanonPicha: Hussein Malla/AP/picture alliance

Ongezeko hilo la vifo limetangazwa na Wizara ya Afya ya Lebanon baada ya watu wasiopungua sita kuuwawa katika shambulio la mapema Jumanne. Vyanzo viwili vya kiusalama kutoka Lebanon vimeeleza kuwa mashambulizi hayo ya anga yalimlenga Kamanda wa Hezbollah nje kidogo mwa mji Mkuu Beirut. Kulingana na vyanzo hivyo Kamanda aliyeuwawa ni Ibrahim Qubaisi.

Hayo yanajiri huku Lebanon ikitangaza kuendelea kuzifunga shule na vyuo kutokana na mashambulizi yanayoendelea.

UN yasisitiza usitishwaji wa mapigano Lebanon

Hatua hiyo imechukuliwa wakati Mashirika ya Umoja wa mataifa yakiutilia mkazo wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa kuzitaka pande zote za mzozo huo kusitisha mapigano na kuhakikisha kuwa zinawalinda raia wa Lebanon.

Umoja wa Mataifa umearifu pia kuwa, maelfu ya watu wamelazimika kuyakimbia makazi yao nchini humo.  Msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa Mathew Saltmarsh amesema  wana wasiwasi mkubwa kutokana na walichokishuhudia kufuatia mashambulizi hayo.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukisisitiza kusimamishwa mapigano Gaza na Lebanon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Picha: BEN MCKAY/AAP/IMAGO

Kwa upande wake msaidizi wa Mwakilishi wa shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa nchini Lebanon Ettie Higgins ameelezea hofu yake hasa kwa upande wa watoto katika vita hivyo akisema kuwa, "Mivutano zaidi katika mzozo huu itakuwa janga kubwa kwa watoto wote wa Lebanon na hasa familia zinazotoka kwenye miji na vijiji vilivyo Kusini na Bekaa, upande wa Mashariki ambako wamelazimika kuyakimbia makazi yao. Watu hawa ambao hawana makazi ni kando ya 112,000 ambao walilazimika pia kuhama makwao tangu Oktoba  mwaka uliopita." 

Mashambulizi zaidi yaripotiwa Gaza, 22 wauwawa

Kwingineko katika Ukanda wa Gaza, watoa huduma za afya wamesema kuwa mashambulizi ya Israel yamewauwa Wapalestina 22 wakati walipokuwa wakipambana na wapiganaji wa Hamas mjini Rafah.

Vifaru vya Israel vimeonekana vikisonga mbele katika upande wa Kaskazini na Magharibi mwa mji huo ulio mpakani na Misri.

Maelfu ya watu wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na mapigano yanayoendelea Lebanon
Foleni za magari zimeshuhudiwa katika mji wa Damour Kusini mwa Lebanon wakati wakaazi wakikimbia mapigano yanayoendeleaPicha: Ibrahim AMRO/AFP

Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, jeshi la Israel lililipua nyumba kadhaa mashariki na katikati mwa mji.

Nao wapiganaji wa Islamic Jihad ambalo ni tawi la Hamas waliwavamia wanajeshi wa Israel walioingia katika eneo hilo kwa kuyalipua mabomu  waliyokuwa wameshayatega.