1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky ayashukuru mataifa ya Ulaya kwa ahadi za misaada

23 Agosti 2023

Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine ametoa shukrani kwa washirika wake barani Ulaya kufuatia ahadi zilizotolewa za msaada mkubwa wa kijeshi na kuzipiga jeki juhudi za kulijenga upya taifa hilo linalopigana vita.

https://p.dw.com/p/4VSvV
Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine
Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine Picha: ROB ENGELAAR/AFP

Akizungumza kupitia hotuba ya kila siku kwa taifa iliyorikodiwa akiwa njiani kurejea nyumbani baada ya kuyatembelea mataifa kadhaa ya Ulaya, Zelensky amesema ahadi zilizotolewa na washirika hao ikiwemo kuipatia Ukraine ndege za kisasa za kivita zitaimarisha ulinzi wa taifa hilo.

Kiongozi huyo alikuwa safarini tangu Jumamosi iliyopita iliyomfikisha Sweden, Uholanzi, Denmark na baadaye Ugiriki kwa mazungumzo na viongozi wa mataifa hayo pamoja na wale wa nchi za kanda ya Balkani aliokutana nao mjini Athens.

Kwenye ziara hiyo, alipokea ahadi ya msaada wa ndege za kivita chapa F-16 kutoka kwa Uholanzi na Denmark huku Ugiriki ikijitolea kuwapa mafunzo marubani wa Ukraine ya kuzirusha ndege hizo mamboleo.