1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu Uganda waadhimisha Iddi wakilaani vita vya Sudan

Mohammed Khelef
21 Aprili 2023

Waumini wa Kiislamu nchini Uganda wameadhimisha sikukuu ya Idd-ul-Fitr huku wakitoa wito wa kukomeshwa kwa mapigano na machafuko nchini Sudan, ambayo wanasema yanasikitisha kwa kuanza katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

https://p.dw.com/p/4QPZD
Uganda Islam l Eid al-Fitr l Zuckerfest
Picha: Lubega Emmanuel /DW

Kuanzia alfajiri ya siku ya Ijumaa (Aprili 21), matamko ya takbiri ndiyo yaliyohanikiza sehemu mbalimbali za mji mkuu wa Uganda, Kampala, na kwingineko wakati Waislamu wakijumuika kwa sala maalum ya Idd-ul-Fitri kusherehekea mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Baada ya sala, maimamu walitoa hotuba zao za kuadhimisha siku ya kwanza tangu kumaliza kwa mfungo, ambapo miongoni mwa mambo wengi, waligusia na kuhimiza amani miongoni mwa jumuiya za Waislamu.

Soma zaidi: Wasudani waadhimisha Eid-ul-Fitr katikati ya mabomu

Hapo ndipo suala la mzozo wa Sudan lilipotajwa kuwa hali inayowasikitisha. "Hili ni jambo la kutufedhehesha waumini wa Kiislamu kwani mzozo huo ulizuka katika mwezi mtukufu wa Ramadhani", alisema Mufti wa Uganda Sheikh Shaban Ramadhan Mubajje, ambaye aliongoza imani kwenye Msikiti Mkuu wa Gaddafi.

Kwa upande wao, waumini mbalimbali waliulezea mwezi wa Ramadhani mwaka huu kuwa kipindi kilichokuwa chenye amani na tofauti na miaka mingine.

'Ramadhani ilikuwa nyepesi'

Licha ya hali ya maisha kuwa ngumu kwa ujumla kwa kila mtu, wengi wa waumini waliozungumza na DW walisema wanashukuru kwa kuweza "kukidhi gharama za chakula."

Uganda Islam l Eid al-Fitr l Zuckerfest
Waumini wa Kiislamu wakihudhuria sala ya Eid-ul-Fitr mjini Kampala, Uganda.Picha: Lubega Emmanuel /DW

Viongozi wa kidini aidha waliwahimiza Waislamu kudumisha tabia njema na mienendo waliodhihirisha katika mwezi wa Ramadhani.

"Hayo ndiyo hasa maisha munayotakiwa kuishi na kuwa mfano kwa watu wa imani nyengine," alisema Sheikh Jamil Maganda aliyeongoza ibada kwenye Msikiti wa Salaam, mtaa wa Ntinda mjini Kampala. 

Soma zaidi: Waislamu kote duniani wanaadhimisha Eid al adha

Kama ulivyo utamaduni wa sikukuu za Iddi kwa Waislamu, nchini Uganda napo familia zimeshuhudiwa zikijumuika kwenye mialiko na kudhihirisha kuwa mandhari ni ya furaha na bashasha.

Serikali ya Uganda illitangaza Ijumaa ya leo (Aprili 21) kuwa siku mapumziko ya kitaifa ili kuwapa nafasi watu kusherehekea Idd-ul-Fitr.

Imeandikwa na Lubega Emmanuel/DW Kampala