1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Ukraine: Tumedunguwa ndege 29 zisizo na rubani za Urusi

Tatu Karema
3 Oktoba 2023

Ukraine imesema Jumanne (3.10.2023) kuwa imezidunguwa takribani ndege 29 zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran pamoja na kombora la masafa marefu lililorushwa na vikosi vya Urusi kutoka Rasi ya Crimea

https://p.dw.com/p/4X4MQ
Wanajeshi wa Ukraine wakiendesha gari la kupambana na ndege zisizo na rubani wakati wa mafunzo ya vita  mjini Kiev
Wanajeshi wa Ukraine Picha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Jeshi la anga la Ukraine limesema kuwa usiku wa kuamkia leo, washambuliaji wa Urusi katika eneo hilo la Crimea, waliishambulia nchi hiyo kwa kutumia ndege hizo zisizo na rubani na kombora aina ya Iskander-K. Taarifa ya jeshi hilo imeeleza kuwa udunguaji huo ulifanywa na vikosi vinavyohusika na eneo la kusini la Mykolaiv na eneo la kati la Dnipropetrovsk.

Ukraine yaonya Urusi inaanzisha kampeini ya mashambulizi dhidi ya miundo mbinu ya nishati

Ukraine imeonya kuwa Urusi inaanzisha upya kampeni ya mashambulizi ya anga dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine ambayo kwenye majira ya baridi kali ya mwaka jana yaliwaacha mamilioni ya watu bila gesi ya kupashia joto nyumba zao na maji kwa muda mrefu.

Soma pia: Shughuli nyingi zimesimama nchini Ukraine tangu Urusi ilipolivamia taifa hilo kijeshi

Wiki hii, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliuhimiza Umoja wa Ulaya kuongeza vikwazo vyake dhidi ya Urusi na pia Iran kwa kupeleka ndege zake zisizo na rubani nchini Urusi.

Jeshi la Urusi halina mipango ya kuwahamasisha wapiganaji zaidi

Shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA, limemnukuu Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, akisema kuwa jeshi la nchi hiyo halina mipango ya kuwahamasisha wanaume zaidi kujiunga katika vita vya Ukraine kwa sababu lina maafisa wa kutosha.

Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu akihudhuria mkutano na waziri wa ulinzi wa China Li Shangfu mjini Moscow mnamo Aprili 18, 2023
Waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu Picha: via REUTERS

Uingereza yasema Urusi yafanikiwa kudhibiti maoni ya umma kwa kutumia jina 'wakala wa kigeni' 

Katika hatua nyingine, wakati wa taarifa zake za kila siku kuhusu vita vya Ukraine, wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema kuwa kura ya maoni iliyofanywa hivi karibuni na kituo cha serikali cha utafiti wa maoni ya umma iligundua kuwa asilimia 61 ya wale waliohojiwa wanachukulia neno "mawakala wa kigeni" kuwa wasaliti wanaoeneza uwongo kuhusu Urusi.

Soma pia:Zelensky: Urefu wa vita nchini Ukraine utategemea msaada wa washirika

Wizara hiyo imesema kuwa hatua za kuitanuwa "Sheria ya Mawakala wa Kigeni" tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, zinapunguza kwa kiasi kikubwa nafasi ya kutolewa kwa habari nchini Urusi na kufanya kuwa vigumu zaidi kutoa maoni yoyote, pamoja na kutofautiana kuhusu vita hivyo hatua ambayo ni kinyume na msimamo rasmi.

Wanaoorodheshwa kama mawakala wa kigeni hukabiliwa na changamoto nyingi

Uingereza inadai mahakama za Urusi zinatumia neno ''wakala wa kigeni'' kama silaha dhidi ya watu binafsi na mashirika.

Mara baada ya kutajwa kuwa wawakala wa kigeni, watu binafsi au mashirika mengi hukabiliwa na changamoto nyingi kwa sababu wanaishia kupoteza wafuasi, biashara, washirika na mapato.

Soma pia:Zelenskiy asema hakuna chochote kitakachodhoofisha harakati zake za kuiangusha Urusi

Walioorodheshwa kama mawakala wa kigeni ni shirika huru la kufuatilia uchaguzi Golos na watu binafsi kama vile mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Dmitry Muratov, huku Kremlin ikiwaandama wakosoaji.