1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUfaransa

Ufaransa yatuma polisi kurejesha utulivu New Caledonia

19 Mei 2024

Ufaransa imewapeleka mamia ya maafisa wa polisi kujaribu kurejesha udhibiti wa njia kuu inayounganisha uwanja wa ndege wa kisiwa cha New Caledonia na mji mkuu Noumea baada ya siku kadhaa za machafuko.

https://p.dw.com/p/4g34M
New Caledonia
Maafisa wa usalama wakisimamia zoezi la kufungua barabara muhimu ya New Caledonia Picha: Delphine Mayeur/AFP

Hayo yametangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X. Zaidi ya polisi 600 pamoja na mgambo 100 wametumwa kuondoa vizuizi vilivyowekwa na makundi ya watu na kuifunga barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 60. 

Machafuko yalizuka mapema wiki hii kwenye kisiwa hicho cha bahari ya Pasifiki kilicho chini ya milki ya Ufaransa kupinga mageuzi ya katiba yanayoshinikizwa na Ufaransa.

Mageuzi hayo yanahusu kuwapatia haki ya kupiga kura watu walioishi kwenye kisiwa cha New Caledonia kwa angalau miaka 10. Makundi ya wazawa wanayapinga mapendekezo hayo wakisema yatapunguza nguvu ya wakaazi wa asili katika ngazi za maamuzi.