1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroLebanon

Kundi la Hezbollah nchini Lebanon laishambulia Israel

Tatu Karema
27 Machi 2024

Kundi la Hezbollah nchini Lebanon limesema limerusha mamia ya makombora kuelekea mji wa mpakani wa Kiryet Shmona nchini Israel mapema siku ya Jumatano.

https://p.dw.com/p/4eAZJ
Mashambulizi ya anga ya Israel katika eneo la Khiam nchini Lebanon
Moshi ukifuka baada ya Israel kufanya mashambulizi ya anga huko Khiam, Lebanon, Februari 7, 2024. Wapiganaji wawili wa Hezbollah na raia mmoja waliuawa.Picha: Taher Abu Hamdan/Xinhua/picture alliance

Mashambulizi hayo ni jibu la mashambulizi makali ya Israel dhidi ya kijiji cha Hebbariyeh Kusini mwa nchi hiyo hapo jana.

Maafisa wawili wa usalama wa Lebanon, wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba takriban watu saba wameuawa katika shambulizi hilo la Israel.

Maafisa hao wameongeza kuwa mashambulizi hayo ya Israel yalionekana kulenga kituo cha huduma za dharura na misaada cha kundi hilo katika kijiji hicho cha Hebbariyeh .

Hakukuwa na tamko la haraka kutoka Israel kuhusu madai hayo ama habari za majeruhi ama uharibifu.

Israel na kundi hilo la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, zimekuwa zikikabiliana katika mashambulizi ya kuvuka mpaka tangu kuzuka kwa vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza, hili likiwa ongezeko kubwa la vita kati ya mahasimu hao wa jadi tangu kuzuka kwa vita kati yao vilivyodumu mwezi mmoja mnamo mwaka 2006.