1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nguo za msaada zinazidisha uchafuzi wa plastiki Kenya

Tatu Karema
16 Februari 2023

Ripoti ya Shirika la Changing Markets Foundation la Uholanzi, imesema thuluthi moja ya nguo za mitumba zilizoingizwa nchini Kenya mwaka 2021 zilikuwa ni kile ilichokiita 'taka za plastiki zilizofichwa'

https://p.dw.com/p/4NZgD
Tansania Dar Es Salaam | Kariakoo Markt | Händler
Picha: Said Khamis/DW

Kila mwaka, tani za nguo za msaada hupelekwa katika mataifa yanayoendelea lakini wastani wa asilimia 30 huishia katika maeneo ya kutupa taka ama kurundikwa katika masoko ya ndani hali inayowezesha kukatizwa kwa utengenezaji wa ndani. Ripoti hiyo, inaonesha kuwa tatizo hilo lina madhara makubwa nchini Kenya, ambako takriban vipande milioni 900 vya nguo zilizotumika husafirishwa kila mwaka. Nguo nyingi zinazosafirishwa kuelekea nchini humo hutengenezwa kutokana na bidhaa za petroli kama vile polyester ama ziko katika hali mbaya hivi kwamba haziwezi kutolewa kama msaada. Nguo hizo huishia kuteketezwa katika maeneo ya kutupa taka karibu na mji mkuu Nairobi na kuwaweka waokotataka wasio rasmi katika hatari ya kuvuta mafusho yenye sumu.

Nguo zinazosombwa katika njia za maji humezwa na wanyama wa majini

Tani za nguo pia husombwa kwenye njia za maji na hatimaye kukatika na kuwa nyuzi ndogo zinazomezwa na wanyama wa majini. Ripoti hiyo inaendelea kusema kuwa zaidi ya kipande kimoja kati ya vitatu vya nguo za mitumba zinazosafirishwa kuingia nchini Kenya ni aina ya plastiki iliyofichwa na suala kuu la uchafuzi wa plastiki wenye sumu nchini.

Bangladesch | Mass Bathing in Buriganga
Uchafuzi wa plastiki wa mazingiraPicha: Mortuza Rashed/DW

Utafiti huo ulitokana na data za forodha, shughuli za mashinani za shirika lisilojipatia faidia la Wildlight pamoja na kikundi cha wanaharakati cha Clean Up Kenya, ambacho kilifanya mahojiano kadhaa. Ripoti hiyo pia ilifichua kuwa baadhi ya nguo hizo zilikuwa na alama za matapishi ama kuharibiwa vibaya huku nyingine zikikosa matumizi katika hali ya joto nchini Kenya.

Nguo nyingi za msaada hazifai kwa matumizi ya ndani

Mwanzilishi wa shirika la Clean Up Betterman Simidi Musasia, ameliambia shirika la AFP kwamba ameshuhudia watu wakifungua marobota ya vifaa vya kuteleza kwenye barafu na nguo za baridi, ambazo hazina manufaa kwa Wakenya wengi. Ripoti hiyo pia imesema kuwa kati ya asilimia 20 na 50 ya nguo zote za msaada hazikuwa za kiwango bora cha kuuzwa katika masoko ya ndani ya mitumba. Nguo zisizovalika huenda zikageuzwa kuwa vitambaa vya kufutia viwandani ama mafuta ya bei nafuu kwa wachoma karanga, kusombwa katika mto Nairobi, kutapakaa katika soko ama kutupwa katika maeneo makubwa ya taka nje ya mji wa Nairobi kama vile eneo la taka la Dandora. Musasia amesema bidhaa hizo zinapaswa kuchaguliwa katika eneo la msaada kabla ya kusafirishwa kuelekea Kenya badala ya kuzituma bila ukaguzi ili kujaribu kuzuia tatizo kutoka kwa chanzo chake.