1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Jovenel Moise wa Haiti auwawa

Saumu Mwasimba
7 Julai 2021

Waziri mkuu asema usalama umeimarishwa kote Haiti na kuwataka wananchi kutulia wakati Jamhuri ya Dominica ikitangaza kuufunga mpaka wake na Haiti

https://p.dw.com/p/3wAa6
Haiti Präsident  Jovenel Moise
Picha: Dieu Nalio Chery/AP Images/picture alliance

Rais Jovenel Moise wa Haiti ameuwawa baada ya makaazi yake ya kibinafsi kushambuliwa hii leo Jumatano. Kaimu waziri mkuu Claude Joseph amewatolea mwito wananchi wa Haiti kuwa watulivu.

Kaimu waziri mkuu Claude Joseph akitoa taarifa ya tukio hilo amesema makaazi ya rais Moise yalishambuliwa leo asubuhi na kiongozi huyo kuuwawa.

"Hatukuwatambua waliohusika, walikuwa wakizungumza Kihispania au Kiingereza. Walishambulia makaazi ya rais wa jamhuri. Rais amefariki kutokana na majeraha. Mkewe hivi sasa anahitaji uangalizi wa madaktari kwa sababu alipigwa risasi.''

Waziri mkuu huyo wa muda ameyataja mauaji hayo ya kiongozi wa nchi kuwa kitendo cha chuki,kisichokuwa cha ubinaadamu na cha kikatili huku akisisitiza kwamba usalama wa nchi umedhibitiwa na jeshi la polisi na jeshi la ulinzi wa taifa.

"Kama waziri mkuu wa sasa naweza kuwahakikishia kwamba muendelezo wa kisiasa serikalini utahakikishiwa.''

Viongozi mbalimbali katika jumuiya ya kimataifa wametoa tamko kulaani mauaji hayo.Rais wa Colombia Ivan Duque amekiita kilichofanyika kuwa kitendi cha uwonga na kuwataka wahaiti waoneshe mshikaman. Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameandika ujumbe wa Twitta akisema ameshtushwa na kuhuzunishwa na mauaji ya rais Moise.Jamhuri ya Dominica imesema inaufunga mpaka wake na Haiti

Symbolbild Gewalt in Haiti
Picha: Jean Mark Herve Abelard/imago images/Agencia EFE

Haiti hata kabla ya kushuhudiwa mauaji haya ya rais wa nchi ilikuwa imeshatumbukia katika hali ya kuongezeka ukosefu wa uthabiti na hasira miongoni mwa wananchi wake kutokana na utawala wa rais Moise. Kiongozi huyo alikuwa akiitawala kwa amri nchi hiyo katika kipindi cha zaidi ya miaka 2 baada ya uchaguzi kushindwa kufanyika,na katika miezi ya karibuni wapinzani walikuwa wakimshinikiza akiuzulu madarakani.

Imeelezwa kwamba majira ya asubuhi kabisa mitaa ya mji mkuu wa  nchi hiyo Port-au Prince kwa sehemu kubwa ilikuwa mitupu,lakini pia inaelezwa kwamba baadhi ya watu walivamia biashara za watu na kuanza kupora katika moja ya maeneo.Waziri mkuu amesema polisi wamepelekwa katika eneo la ikulu na kwenye maeneo mengine.

Ikulu ya Marekani imeshatoa tamko kuhusu hali hiyo nchini Haiti ikisema shambulio lililomuua rais Moise ni kitendo cha kutisha na cha kusikitisha na kwamba bado inakusanya taarifa kuhusu kilichotokea.Kwa mujibu wa katibu wa habari wa ikulu Jen Psaki rais Joe Biden atapewa ripoti baadae Jumatano na timu yake ya usalama wa taifa. Lakini pia ameongeza kusema kwamba Marekani imejiweka tayari na iko pamoja na watu wa Haiti katika kuwapa msaada wanaohitaji.

Haiti Präsident  Jovenel Moise
Picha: Dieu Nalio Chery/AP/picture alliance

Ikumbukwe kwamba upinzani nchini Haiti uliwahi kuilaumu Marekani ambayo ni mfadhili mkubwa wa Haiti,kwa kumvumilia sana rais Moise kutokana na kuonesha kuunga mkono sera ya kigeni ya Marekani.Viongozi wa upinzani walimtuhumu rais Moise aliyekuwa na umri wa miaka 53 kwamba alitaka kujiongezea madaraka kwa kupitisha amri ya kupunguza nguvu za mahakama inayohusika kukagua mikataba ya serikali na kuunda idara maalum ya ujasusi inayopokea amri kutoka kwa rais tu.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhaririri: Grace Patricia Kabogo