1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUrusi

Putin: Sina mpango wa kushambulia mataifa ya NATO

Sylvia Mwehozi
28 Machi 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin amenukuliwa akisema kuwa hana dhamira ya kushambulia taifa lolote mwanachama wa Jumuiya ya NATO lakini akaonya ikiwa Mataifa ya Magharibi yataipatia Ukraine ndege za F-16, zitadunguliwa.

https://p.dw.com/p/4eDCO
 Vladimir Putin| Urusi
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Sputnik/via REUTERS

Akizungumza na marubani wa jeshi la anga la Urusi, Putin alisema kuwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani, umejipanua kuelekea upande wa mashariki mwa Urusi tangu kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991, lakini Moscow haikusudii kushambulia nchi yoyote ya NATO.

"Huu ni ujinga mtupu. Uwezekano wa kushambulia nchi nyingine, Poland, mataifa ya Baltiki na pia imewaogopesha raia wa Jamhuri ya Czech, ni ujinga tu!. Ni njia nyingine ya kudanganya wananchi wao na kuchota pesa zaidi kutoka kwao, kuwalazimisha kubeba mzigo huo"

F-16
Ndege za kivita za Marekani za F-16Picha: Sgt. Heather Ley/U.S. Air Force/AP Photo/picture alliance

Alipoulizwa kuhusu ndege za kivita za F-16ambazo Mataifa ya Maghaibi yameahidi kuipatia Ukraine, Putin alidokeza kuwa ndege za namna hiyo haziwezi kubadili hali ya mambo huko Ukraine. Alisema kama watazipeleka na wanazungumzia kuwafunza marubani, wajue kwamba hakuna chochote kitakachobadilika kwenye uwanja wa mapambano.

"Na tutazidungua ndege hizo kama ambavyo hivi sasa tunateketeza vifaru, magari ya kijeshi na vifaa vingine, ikiwa ni pamoja na mifumo tofauti ya kurusha makombora".Urusi na Ukraine waendelea kushambuliana

Kauli ya Putin inafuatia matamshi yaliyotolewa jana na waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba kwamba ndege hizo zinapaswa kuwasili Ukraine ndani ya miezi michache ijayo.

Tukiweka kando suala hilo, vikosi vya Ukraine vimedai kudungua droni 26 kati ya 28 zilizorushwa na Urusi katika shambulio la usiku wa kuamkia leo. Jeshi la Kyiv limesema Droni hizo zilizotengenezwa Iran zimeharibiwa katika baadhi ya maeneo ya mashariki na kusini mwa Ukraine. Urusi imekuwa ikifanya mashambulizi ya mara kwa mara ya anga katika maeneo ya makazi ya raia katika uvamizi wake wa miaka miwili huko Ukraine.

Hannover Messe 2005 | Putin na Schröder
Kansela wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schröder na PutinPicha: R. Jensen/dpa/picture-alliance

Na Kansela wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schröderamesema kuwa bado anafikiria urafiki wake na rais Putin unaweza kuchangia kumaliza vita vyake na Ukraine. Kansela huyo wa zamani ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Ujerumani DPA, akiongeza kuwa wamefanya kazi pamoja kwa busara kwa miaka mingi. "Labda hilo bado linaweza kusaidia kupata suluhisho la mazungumzo, sioni njia nyingine yoyote."

Schröder amekuwa na usuhuba na Putin tangu alipokuwa Kansela wa Ujerumani kutoka mwaka 1998 hadi 2005 na ameendelea kufanya kazi na kampuni nyingi za Urusi za mabomba ya gesi ya Nord Stream kupitia Bahari ya Baltiki. Ingawa kiongozi huyo wa zamani wa Ujerumani ameelezea shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine kama "kosa baya" lakini hajawahi kumkataa Putin.