1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Mpango wa usafirishaji nafaka za Ukraine waongezewa muda

Iddi Ssessanga
18 Machi 2023

Maafisa wamesema mpango wa kihistoria wa wakati wa vita unaoruhusu usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine umeongezewa muda wake. Lakini haijabainishwa wazi mpango huo umerefushwa kwa muda gani.

https://p.dw.com/p/4OtAt
Ukraine | Getreideernte
Picha: Alexey Furman/Getty Images

Mpango wa wakati wa vita usiokifani ambao unaruhusu nafaraka kutiririka kutoka Ukraine kwenda mataifa barani Afrika, Mashariki ya Kati na Asia ambako njaa ni kitisho kinachoongezeka na bei za chakula zikiwasukuma watu zaidi katika umaskini umerefushwa, maafisa wamesema Jumamosi.

Urefushwaji huo umetangazwa na Umoja wa Mataifa na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, lakini hakuna kati yao aliethibitisha muda wa urefushaji huo.

Soma pia: Erdogan atangaza kurufeshwa kwa mkataba wa nafaka kupitia bahari nyeusi

Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine Oleksandr Kubrakov alitweet kwamba mpango huo umeongezewa siku 120 - urefu ambao Ukraine, Uturuki na Umoja wa Mataifa walikuwa wanataka. Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka Urusi, ambayo ilitaka kufanya upya kwa siku 60.

Türkei I Getreidefrachter  auf Durchfahrt durch Bosporus
Meli yenye bendera ya Liberia, Asl Tia ikiwa njia kwenda China, ikivuka daraja la Bosphorous ikiwa na tani 39,000 za unga wa ufuta kutoka Ukraine. Novemba 02, 2022.Picha: Chris McGrath/Getty Images

Huu ni urefushaji wa pili wa mikataba tofauti ambayo Ukraine na Urusi zilitia saini na Umoja wa Mataifa na Uturuki kuruhusu chakula kuondoka katika eneo la Bahari Nyeusi baada ya Urusi kuvamia jirani yake zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Mataifa hayo yanayopigana ni wauzaji wakuu wa kimataifa wa ngano, shayiri, mafuta ya alizeti na bidhaa nyingine za bei nafuu za chakula ambazo mataifa yanayoendelea yanategemea.

Urusi imelalamika kwamba usafirishaji wa mbolea yake - pia muhimu katika mfumo wa chakula duniani - kutofika masoko ya kimataifa, ambalo kwa muda mrefu limekuwa suala chini ya makubaliano yalioanza kutekelezwa mwezi Agosti na kurefushwa kwa miezi minne mingine mwezi wa Novemba.

Soma pia: Mkataba wa usafirishaji nafaka za Ukraine waongezwa muda wa siku 60

Vita nchini Ukraine vilisukuma bei za vyakula juu hadi kuweka rekodi ya kupanda mwaka jana na kuchochea mzozo wa chakula duniani pia unaohusishwa na athari za janga la COVID-19 na sababu za mabadiliko ya tabianchikama ukame.

Usumbufu huo wa usafirishaji wa nafaka zinazohitajika kwa ajili ya chakula kikuu katika maeneo kama vile Misri, Lebanon na Nigeria ulizidisha changamoto za kiuchumi na kusaidia kuwasukuma mamilioni ya watu zaidi katika umaskini au uhaba wa chakula. Watu katika nchi zinazoendelea wanatumia pesa zao zaidi kwenye mambo ya msingi kama vile chakula.

Türkei Ankara | Präsident Recep Tayyip Erdogan gibt neuen Wahltermin im Mai bekannt
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametangaza kurefushwa kwa makubaliano ya usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine, yaliokuwa yamalizike muda wake Machi 18.Picha: Alo Eren Kaya/AFP

Changamoto kwa mataifa maskini

Bei ya chakula imeshuka kwa muda wa miezi 11 mfululizo, lakini chakula kilikuwa tayari ghali kabla ya vita kwa sababu ya ukame kutoka Amerika hadi Mashariki ya Kati - ulioharibu zaidi katika Pembe ya Afrika, na maelfu wakifa Somalia. Mataifa maskini ambayo yanategemea chakula kutoka nje kwa bei ya dola yanatumia zaidi huku sarafu zao zikidhoofika.

Soma pia: Uturuki inapanga kurefusha mpango wa usafirishaji nafaka

Mgogoro huo umewaacha takriban watu milioni 345 wakikabiliwa na uhaba wa chakula, kulingana na Mpango wa Chakula Duniani wa Umoja wa Mataifa.

Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi umesaidia kwa kuruhusu tani milioni 24 za nafaka kuondoka kwenye bandari za Ukrainia, huku asilimia 55 ya shehena zikielekea katika mataifa yanayoendelea, Umoja wa Mataifa ulisema.

Mikataba hiyo pia imekabiliwa na vikwazo tangu iliposimamiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki: Urusi ilijiondoa kwa muda mfupi mwezi Novemba kabla ya kujiunga tena na kuongeza muda wa makubaliano hayo. Katika miezi michache iliyopita, ukaguzi uliokusudiwa kuhakikisha meli hubeba nafaka pekee na sio silaha zimepungua.

Meli ya UN iliyobeba nafaka yaelekea Afrika kutoka Ukraine

Hilo limesaidia kusababisha mlundikano wa meli zinazongoja katika bahari ya Uturuki na kupungua kwa kiasi cha nafaka kutoka Ukraine hivi karibuni. Ukraine na baadhi ya maafisa wa Marekani wameilaumu Urusi kwa kupungua kwa mtiririko wa meli, jambo ambalo nchi hiyo inakanusha.

Soma pia: Urusi yarudi katika mkataba wa kusafirisha nafaka za Ukraine

Wakati mbolea imekwama, Urusi imekuwa ikiuza nje kiasi kikubwa cha ngano baada ya mauzo hayo kushuka kwa kiwango kilichoweka rekodi. Takwimu kutoka taasis ya data za kifedha ya Refinitiv zinaonyesha kuwa ngano ya Urusi imeuzwa zaidi ya mara mbili hadi tani milioni 3.8 mwezi Januari ikilinganishwa kipindi sawa na hicho mwaka uliopita, kabla ya uvamizi.

Usafirishaji wa ngano ya Urusi ulikuwa wa kiwango cha juu au karibu na Novemba, Desemba na Januari, na kuongezeka kwa asilimia 24 zaidi ya miezi mitatu iliyopita, kulingana na Refinitiv. Ilikadiria Urusi ingeuza nje tani milioni 44 za ngano mnamo 2022-2023.

Chanzo: APE