Vita vya siku 6 vyatoa vizazi vya mamilioni ya wakimbizi
6 Juni 2017Katika mkesha wa miaka 50 baada vita hivyo vya Mashariki ya Kati vilivyodumu kwa siku sita, Guterres amesema Israel bado inakalia Ukingo wa Magharibi, Jerusalem Mashariki, na Milima ya Golan ya Syria na hilo limesababisha kile alichokitaja kuwa "mzigo mkubwa wa kibinidamu na kimaendeleo".
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kwa Israel kuendelea kuyakalia maeneo ya Wapalestina kunapelekea kuwepo kwa ghasia zinazojirejelea, na kutuma ujumbe kwa Wapalestina kuwa kujitawala ni ndoto tu na kwa Waisraeli inatuma ujumbe kuwa amani ni jambo lisiloweza kufikiwa.
Guterres amesema kukoma kwa mzozo wa tangu jadi kati ya Isreal na Palestina kutafungua milango ya ushirikiano na usalama.
Kauli yake imeungwa mkono na Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad al-Hussein, ambaye ametoa wito wa kusitishwa kukaliwa kwa maeneo ya Wapalestina akisema hilo litazinufaisha pande zote mbili na kukomesha uhasama wa miaka 50.
Katika hotuba ya ufunguzi wa kikao cha wiki tatu cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne (Juni 6), al-Hussein alisema Wapalestina wanaadhimisha "nusu karne ya mateso makubwa" kwa kukaliwa kimabavu na kuongeza Waisraeli pia wanastahili kujinasua kutoka ghasia, akionya kuendelea kwa uhasama "kunamaanisha kuendelea kwa machungu kwa pande zote mbili."
Netanyahu asema amani ya Israel ndilo la kwanza
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Israel itadumisha udhibiti wa eneo lote la Ukingo wa Magharibi ama pakiwepo au pasiwepo kwa makubaliano ya amani na Wapalestina.
Akizungumza jana katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 tangu Israel iliposhinda vita hivyo, Netanyahu alisema nchi yake inatafuta amani ya kweli na majirani zake lakini wakati huo huo sharti ihakikishe usalama wake.
Katika vita hivyo vya siku sita, Israel ilizishinda Misri, Syria na Jordan, ikayachukua maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki kutoka Jordan, Ukanda wa Gaza na Rasi ya Sinai kutoka Misri na Milima ya Golan kutoka Syria.
Baadaye iliirejesha Rasi ya Sinai kwa Misri baada ya makubaliano ya amani kati yao yaliyofikiwa 1979. Mnamo 2005 iliwaondoa walowezi na majeshi yake kutoka Ukanda wa Gaza unaodhibitiwa hivi sasa na kundi la wanamgambo la Hamas.
Mwandishi: Caro Robi/AFP/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga