1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Marekani na Uingereza yashambulia mji wa bandari wa Hodeidah

23 Machi 2024

Kiongozi wa kamati kuu ya mapinduzi ya Yemen Muhammad Ali Al-Houthi amesema kumekuwepo kwa mashambulizi aliyoyaita ya "kiholela" yaliofanywa na Marekani na Uingereza katika mji wa bandari wa Hodeidah nchini Yemen.

https://p.dw.com/p/4e35y
Meli iliyotia nanga kwenye bandari ya Hodeidah, Yemen.
Meli iliyotia nanga kwenye bandari ya Hodeidah, Yemen.Picha: nieyunpeng/Xinhua/picture alliance

Al-Houthi ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa, mashambulizi hayo ya Marekani na Uingereza yanalenga kuondoa kizuizi cha majini dhidi ya meli zenye mafungamano na Israel.

Shirika la habari la Saba linaloendeshwa na waasi wa Houthi limeripoti kuwa, ndege za Marekani na Uingereza zimefanya mashambulizi kwenye mji wa bandari wa Hodeidah katika bahari ya Sham.

Soma pia: Marekani yashambulia maeneo ya Wahotuhi wa Yemen 

Tangu katikati ya mwezi Novemba, waasi wa Houthi wamefanya mashambulizi ya mara kwa mara kuzilenga meli za kimataifa katika bahari ya Sham ambayo ni njia muhimu ya biashara ya kimataifa.

Wahouthi wamesema wanazishambulia meli zenye mafungamano na Israel ili kuonyesha mshikamano na Wapalestina.