1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuipelekea Ukraine vifaru chapa M1 Abrams

25 Januari 2023

Katika kile kitakachokuwa kubadilika kwa msimamo, serikali ya rais wa Marekani Joe Biden inatarajiwa kutoa ridhaa ya kutumwa kwa vifaru chapa M1 Abrams kwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Meu5
USA Panzer M1A2 Abrams
Picha: piemags/IMAGO

Haya yamesemwa na maafisa wa Marekani wakati ambapo hatua ya jamii ya kimataifa kusitasita kuipelekea Ukraine vifaru vya kivita, ikionekana kuanza kupwaya.

Uamuzi wa Marekani kutuma zaidi ya vifaru 30 huenda ukatangazwa mapema, hata Jumatano, ingawa huenda ikachukua miezi kwa vifaru hivyo kuwasili Ukraine. Afisa mmoja amesema vifaru hivyo vitanunuliwa kutokana na mfuko wa fedha za msaada wa kujilinda inazopewa Ukraine.

Inaarifiwa kwamba itachukua miezi au hata miaka kwa vifaru hivyo kufika Ukraine na majeshi ya nchi hiyo kupewa mafunzo ya jinsi ya kuvitumia.

Pentagon yakataa kuthibitisha kupelekwa kwa M1 Abrams Ukraine

Tangazo hilo la Marekani linatarajiwa kutolewa pamoja na tangazo la Ujerumani la kuidhinisha ombi la Poland la kutaka kupeleka vifaru chapa Leopard 2 nchini Ukraine.

USA M1 Abrams Panzer
Jeshi la Marekani likifanya luteka Jordan na vifaru M1 AbramsPicha: piemags/IMAGO

Maafisa wa Marekani walikuwa wamesema kwamba vifaru hivyo chapa M1 Abrams ni ghali kuvidumisha na ni vigumu kuwapa mafunzo majeshi ya Ukraine kuvitumia na vinaendeshwa na mafuta ya ndege mambo yanayofanya vifaru hivyo kutokuwa chaguo sahihi kwa awamu hii ya vita nchini Ukraine.

Wizara ya ulinzi ya Marekani imekataa kuthibitisha iwapo itapelekea vifaru hivyo Ukraine. Jenerali Pat Ryder ni msemaji wa Pentagon.

"Sina cha kutangaza leo kuhusiana na vifaru vya M1. Nafikiri kama tulivyokuwa tukisema kila mara, tunaendelea kufanya majadiliano na Ukraine na marafiki zetu wa kimataifa na washirika, tukijikita katika matakwa ya sasa ya haraka katika eneo la mapigano. Ila tuna majadiliano pia kuhusiana na kile watakachokihitaji kwa baadae na tutaendelea kuwa na majadiliano hayo," alisema Ryder.

Kwa kukubali kuvipeleka vifaru hivyo katika muda ambao haujawekwa wazi bado, Marekani sasa imetimiza masharti ya Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani aliyetaka ionyeshe dhamira ya kweli kabla Ujerumani haijapeleka vifaru vyake chapa Leopard 2 Ukraine.

Kansela Scholz kulihutubia bunge Jumatano

Duru zilizo karibu na suala hilo zinasema uamuzi huu wa Marekani ni sehemu ya majadiliano iliyokuwa nayo na Ujerumani kuhusiana na kusitasita kwake kuvipeleka vifaru vyake na pia kuonyesha umuhimu wa dhamira yake.

Deutschland, Berlin | Regierungserklärung von Olaf Scholz im Bundestag
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Maafisa katika serikali ya Ujerumani wamekataa kutoa tamko lolote kuhusiana na makubaliano hayo ya kupeleka vifaru. Lakini gazeti la kila wiki nchini Ujerumani la Der Spiegel, hapo jana liliripoti bila kutaja chanzo, kwamba, Ujerumani itaipelekea Ukraine angalau vifaru 15 vya Leopard 2 kutoka kwenye hifadhi yake ya kijeshi.

Kansela Olaf Scholz anatarajiwa kulihutubia bunge Jumatano na kujibu maswali ya wabunge ambao wamekuwa wakiishinikiza serikali kujiunga na marafiki zake kupeleka vifaru hivyo Ukraine.

Chanzo: Reuters/AP