1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJamhuri ya Kongo

Mapigano yaendelea mji wa Kitshanga Kongo

6 Novemba 2023

Mapigano makali yametokea tangu asubuhi ya jana Jumapili karibu na mji wa kimkakati wa Kitshanga wilayani Masisi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4YRQ4
Mpiganaji wa kundi la M23 akiwa katika doria
Mpiganaji wa kundi la M23 akiwa katika doriaPicha: GLODY MURHABAZI/AFP via Getty Images

Waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na jeshi la Rwanda walifaulu kuudhibiti tena mji wa Burungu pamoja na Kijiji cha Kabalekasha baada ya kuwafukuza wapiganaji Wazalendo waliokalia miji hiyo kwa zaidi ya mwezi moja. 

Vyanzo vya ndani vimeeleza kuwa waasi hao wa M23 walizishambulia ngome za vijana wapiganaji wazalendo kwenye miji hiyo ya Burungu na Kabalekasha karibu na mji wa Kitshanga waliyoidhibiti wiki moja iliyopita.

Mashirika ya kiraia katika eneo hilo lenye utajiri wa madini yalithibitisha kuingia miji hiyo mikononi mwa kundi la M23 na kukatiza shughuli kwenye njia muhimu inayotumika kusambaza vyakula katika mji wa Goma.

Soma pia:Jeshi Kongo lakabiliana na mashambulizi ya M23

Milio ya risasi iliyofwatiwa na mlolongo wa makombora, ilisabisha mamia ya raia walioanza kurejea Burungu kukimbia tena na kwenda kujihifadhi katika kambi za umoja wa mataifa mjini Kitshanga.

Silaha nzito zatumika katika mapambano

Milio ya silaha nzito imesikika pia katika miji ya Kibati na Buhumba iliyo umbali wa karibu kilometa 20 na mji wa Goma ambako wapiganaji wazalendo wanapambana na M23 kwenye ngome yao muhimu ya Kanyabuki wilayani Nyiragongo.

Ni vigumu hadi sasa kuelezea ni nani anayedhibiti eneo hilo wakati mapigano yakiendele.

Vita vya M23 vinaathiri pia wakazi wa Bukavu

Utawala wa rais Felix Tshisekedi umesisitiza kwamba jeshi lake halijafanya mashambulizi yoyote katika miezi ya hivi karibuni na kwamba ni makundi huru ya wapiganaji ndio yanayopigana na waasi wa M23.

Soma pia:Mapigano yaibuka Kongo kati ya M23 na vijana wazalendo

Haya yanajiri wakati huu ambapo kikosi cha walinda amani wa umoja wa mataifa, MONUSCO kilizindua wishoni mwa juma lililopita operesheni ya Springbok inayo lenga kuulinda mji wa Goma na mji wa Sake, hasa kutokana na tishio la mashambulizi kutoka kwa waasi wa M23, operesheni inayoanza kupingwa na miungano ya kiraia.