1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mackenzie kusalia kizuizini miezi sita zaidi

Grace Kabogo
19 Septemba 2023

Mahakama ya Shanzu mjini Mombasa nchini Kenya imeamuru kuendelea kuzuiliwa kwa mshukiwa wa mauaji ya halaiki katika msitu wa Shakahola, Paul Mackenzie, kwa siku 180 zaidi na hivyo atasalia kizuizini kwa miezi sita.

https://p.dw.com/p/4WXot
Kenia Kilifi | Exhumierung von Mitgliedern von Christlichem Kult durch Polizei
Picha: Stringer/REUTERS

Mahakama ilisema siku ya Jumanne (Septemba 19) kwamba kuzuiliwa kwa mshukiwa huyo ni kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wa kesi inayomkabili yeye na wenzake 29 wanaotuhumiwa kusababisha vifo vya mamia ya watu kwa kuwashauri wajizuwie kula na kunywa hadi kufa. 

Takriban watu 429 waliripotiwa kufariki kutokana na kutii amri hiyo, na miili yao ilifukiliwa kutoka kwenye Msitu wa Shakahola katika Kaunti ya Kilifi.

Soma: Uchunguzi wa maiti za maafa ya msitu wa Shakahola waanza

Upande wa mashitaka uliiambia mahakama hiyo kuwa haukuwa umekusanya ushahidi wa kutosha. 

Kulingana na upande wa mashtaka, miili 360 kati ya iliyofukuliwa ilikuwa imeoza sana. 

Zoezi la kufukuwa makaburi, ambalo limesitishwa kwa sasa, lilikuwa likifanyika kwa awamu.

Shauri hilo litasikilizwa tena tarehe 12 mwezi Oktoba.