1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaLibya

Libya: Zaidi ya miili 5,300 imehesabiwa

Grace Kabogo
13 Septemba 2023

Serikali ya upande wa Mashariki ya Libya imesema zaidi ya miili 5,300 imehesabiwa Derna baada ya mji huo kukumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Daniel na kwamba idadi hiyo inaweza ikaongezeka maradufu.

https://p.dw.com/p/4WHIq
Libyen | Überschwemmung und Hochwasser in Derna
Mji wa Derna ulioathiriwa na mafurikoPicha: Abdullah Mohammed Bonja/AA/picture alliance

Waziri anayehusika na usafiri wa anga katika serikali ya Mashariki ya Libya Hichem Abu, amesema mawimbi ya bahari yamekuwa yakiipeleka ufukweni baadhi ya miili. Amesema timu za uokozi zimekuwa zikifanya kazi usiku na mchana kuitafuta miili mingine ambayo imetapakaa mitaani na ile iliyokwama chini ya vifusi.

IOM: Watu 30,000 wamekimbia makaazi yao

Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji, IOM, limesema zaidi ya watu 30,000 wameyakimbia makaazi yao kwenye mji wa Derna, ambao umeathiriwa zaidi na kimbunga hicho.

Kwa mujibu wa IOM, inafahamika pia watu wengine 6,085 wameyakimbia makaazi yao kwenye miji mingine iliyokumbwa na kimbunga ikiwemo Benghazi. IOM na washirika wake wanaratibu shughuli ya kupeleka mara moja dawa, na vifaa vinavyotumika kuwatafuta na kuwaokoa watu pamoja na wafanyakazi kwenye maeneo yaliyoathiriwa.

Libyen | Überschwemmung und Hochwasser in Libyen
Timu ya Hilali Nyekundu ya Libya wakiratibu juhudi za kutoa misaadaPicha: LIBYAN RED CRESCENT AJDABIYA/REUTERS

Aidha, mjumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, IFRC nchini Libya, Tamer Ramadan amesema zaidi ya watu 40,000 wameyakimbia makaazi yao kwenye mji wa Derna. Ramadan amesema wana timu mbili ambapo moja inaratibu juhudi za kutoa misaada.

''Tuna timu ya Hilali Nyekundu ya Uturuki, hivi karibuni tutakuwa na timu ya Hilali Nyekundu kutoka Kuwait. Pia tunapeleka timu ya wataalamu wa IFRC kuwasaidia wenzetu wa Hilali Nyekundu ya Libya, kutathmini, usimamizi wa operesheni kwenye maeneo yaliyoahirika," alifaanua Ramadan.

Ramadan amesema pia mashirika ya misaada na masuala ya kiutu yatatoa ombi la kimataifa hivi karibuni kwa lengo la kusaidia kufadhili mahitaji makubwa huko Derna na miji mingine iliyoathiriwa na mafuriko mashariki mwa Libya.

Marokko Erdbeben Marakesch
Jengo lililoharibiwa na tetemeko la ardhi kwenye mji wa Moulay Brahim, MoroccoPicha: Khaled Nasraoui/dpa/picture alliance

Umoja wa Mataifa kwa upande wake unakusanya misaada kwa ajili ya watu walionusurika na mafuriko hayo nchini Libya na kwamba umoja huo unashirikiana na watu ndani ya Libya na washirika wake wa kimataifa kupata msaada wa dharura wa kibinadamu utakaopelekwa katika maeneo yaliyoathirika nchini humo.

Mfalme wa Morocco awatembelea majeruhi wa tetemeko la ardhi

Wakati huo huo, Mfalme Mohammed VI wa Morocco jana aliwatembelea baadhi ya majeruhi wa tetemeko la ardhi ambalo lilipiga nchini humo wiki iliyopita na kusababisha vifo vya takribani watu 2,900.

Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti kuwa Mfalme Mohammed VI aliitembelea hospitali ya Chuo Kikuu cha Marrakesh na kuonesha mshikamano kwa taifa lake, ambapo pia alichangia damu.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema hakuna haja ya kuendelea kwa mjadala kuhusu hali ya uhusiano wa Ufaransa na Morocco kuhusu suala la misaada kwa wahanga wa tetemeko la ardhi. Morocco haijaukubali msaada wa Ufaransa, hali inayozusha maswali kuhusu mvutano baina ya serikali hizo mbili.

 

(AFP, AP, Reuters)