1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Kyiv yadai kuishambulia kambi ya Urusi huko Crimea

30 Oktoba 2023

Ukraine imesema hii leo kwamba imeishambulia Kambi ya Jeshi la Anga la Urusi iliyopo kwenye rasi ya Crimea, ikitumia makombora na boti zinazoendeshwa kwa rimoti.

https://p.dw.com/p/4YCnQ
Picha kutoka juu ikionesha moja ya mashambulizi huko Crimea wiki za karibuni
Rasi ya Crimea imekuwa kitovu cha mapambano kati ya Urusi na Ukraine Picha: PLANET LABS PBC/REUTERS

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na vikosi vya Ukraine imesema kambi muhimu ya jeshi la anga ya Urusi iliyo kwenye mwambao wa magharibi wa rasi ya Crimea ndiyo imelengwa kwa makombora.

Duru za habari zimearifu juu ya kutokea shambulizi katika kijiji la Olevinka eneo lililo karibu na kambi hiyo ya jeshi. Ripoti zinasema makombora ya Marekani cha ATACMS ndiyo yalitumika kufanya shambulizi hilo lililowajeruhiwa wanajeshi 17 na kuharibu magari matano.

Hadi sasa Urusi haijathibitisha shambulio hilo lakini Gavana wa mji wa bandari huko Crimea wa Sevastopol, Mikhail Razvozhayev, ameandika kupitia ukurasa wa mtandao wa Telegram kuwa kamandi ya jeshi la majini la Urusi iliyopo kwenye eneo la Bahari Nyeusi ilizima shambilizi la droni usiku wa kuamkia leo.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi pia imearifu juu ya mashumbulizi mengi yaliyozimwa leo mchana yakiilenga rasi ya Crimea.

Crimea bado kitovu cha mapambano kati ya Urusi na Ukraine

Ukraine imekuwa ikilenga kuhujumu shughuli za kijeshi za Urusi kwenye rasi Crimea inayotumiwa kwa sehemu kubwa na Moscow kuratibu upelekeaji silaha na mahitaji mengine kwa wanajeshi wake wanaopigana ndani ya Ukraine.

Shambulio dhidi ya daraja la Crimea mnamo mwezi Agosti
Shambulio dhidi ya daraja la Crimea mnamo mwezi Agosti Picha: Alyona Popova/TASS/dpa/picture alliance

Rasi hiyo iliyochukuliwa kwa mabavu na Urusi kutoka mikononi mwa Ukraine mnamo mwaka 2014 imekuwa kitovu cha makabiliano baina ya pande hizo mbili katika miezi ya karibuni.

Wakati huo huo Ukraine imeripoti leo kwamba Urusi inaimarisha vikosi vyake kwenye mji Bakhmut ulio mashariki mwa Ukraine ambao umeharibiwa kwa vita.

Kamanda mmoja wa jeshi la Ukraine amesema Moscow imebadili safu ya vikosi vyake na kuviweka tayari kwa mapambano badala ya hali ya kujilinda iliyoshuhudiwa wiki za karibuni.

Urusi iliukamata mji wa Bakhmut baada ya mapigano makali na vikosi vya Ukraine lakini tangu mwezi Juni wanajeshi wa Kyiv wanaendesha kampeni kali ya kijeshi kujaribu kuukamata tena mji huo.

Urusi yainyooshea kidole cha lawama Ukraine uvamizi wa Uwanja wa Ndege wa Dagestan 

Waandamanaji waliokuwa wakipaza sauti dhidi ya Wayahudi walipovamia uwanja wa ndege wa Makhachkala katika jimbo la Urusi la Dagestan.Picha: AP/
Waandamanaji waliokuwa wakipaza sauti dhidi ya Wayahudi walipovamia uwanja wa ndege wa Makhachkala katika jimbo la Urusi la Dagestan.Picha: Ramazan Rashidov/TASS/dpa/picture alliance

Hayo yanajiri katika wakati nchi hizo mbili zilizo vitani zimetumbukia hii leo kwenye mzozo mpya. Urusi imeituhumu Ukraine kuwa nyuma ya mkasa wa waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina kuuvamia uwanja wa ndege wa jimbo la kusini mwa Urusi la Dagestan hapo jana jioni.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Urusi Maria Zakharova amesema utawala mjini Kyiv ulikuwa na dhima ya moja kwa moja kwenye kisa hicho kilichoshuhudia mamia ya watu wakivunja vizuizi vya uwanja wa ndege wa Makhachkala kwenda kuwatafuta abiria wa kiyahudi waliwasili kwa ndege iliyotua kwa muda kutokea Tel Aviv ikielekea Moscow.

Kwa upande wake msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov hakuitaka Ukraine moja kwa moja lakini amesema kile kilichotokea Dagestan ni mpango kutoka nje.

"Inafahamika na ni jambo la wazi kwamba matukio ya jana kwenye uwanja wa ndege wa Makhachkala ni matokeo ya mkono kutoka nje, na kwa hakika inatokana na ushawishi wa kigeni. Ni dhahiri kuutokana na picha za televisheni zinavyoonesha kinachoendelea Ukanda wa Gaza, vifo vya watoto, wazee madaktari na wengine, ni rahisi wale wenye nia mbaya kuitumia nafasi hiyo na kuzusha vurumai" amesema Peskov.

Ukraine haijasema chochote bado kuhusu tuhuma hizo. Viongozi wa Dagestan ikiwemo gavana wake wamekaririwa wakisema waratibu wa waandamanaji waliendesha mipango yao kupitia mtandao wa Telegram wakiwa ndani ya ardhi ya Ukraine.