1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Kiongozi wa upinzani Chad auawa katika shambulizi

Bruce Amani
29 Februari 2024

Mpinzani mkuu wa watawala wa kijeshi nchini Chad, Yaya Dillo Djerou ameuawa katika shambulizi la kijeshi lililofanywa kwenye makao makuu ya chama chake.

https://p.dw.com/p/4d2Uc
Kiongozi wa upinzani Chad Yaya Dillo.
Chad imethibitisha kuuawakwa Yaya Dillo, ambaye pia ni binamu yake rais wa mpito Mahamat Deby.Picha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Msemaji wa serikali ambaye pia ni waziri wa mawasiliano Abderaman Koulamallah amesema Dillo alifariki jana, katika ofisi za chama chake ambako alikuwa amejifungia.

Hakutaka kujisalimisha na aliwafyatulia risasi askari. Mwendesha mashitaka mkuu awali alisema watu kadhaa wlaifariki akiwemo Yaya Dillo, bila kutoa maelezo ya mazingira ya vifo hivyo.

Chad | Uwepo wa kijeshi mjini N'Djamena
Wanajeshi wakilinda usalama mjini N'Djamena kufuatia kile kilichotajwa kuwa jaribio la mapinduzi.Picha: AFP/Getty Images

Dillo, ambaye alikiongoza chama cha upinzani cha Socialist Party Without Borders - PSF, alituhumiwa kwa kuongoza shambulizi kwenye ofisi za usalama wa ndani usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano.

Soma pia: Serikali ya Chad yatangaza tahadhari baada ya shambulizi kwenye idara ya usalama

Akizungumza na AFP jana, Dillo alikanusha kuhusika kwa vyovyote na tukio hilo, akiyataja madai hayo kuwa ni ya uwongo na yanayochochewa kisiasa.

Chad ilitangaza Jumanne kuwa uchaguzi wa rais utafanyika Mei 6, ambapo rais wa mpito Mahamat Idriss Deby Itno na Dillo ambaye ni binamu yake, walipanga kugombea.