1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Hamas awasili Cairo kujadili hali ya Gaza

Iddi Ssessanga
20 Februari 2024

Kiongozi mkuu wa Hamas Ismail Haniyeh amewasili mjini Cairo kwa ajili ya mazungumzo na maafisa wa Misri, siku kadhaa baada ya wapatanishi kusema matarajio ya mapatano mapya ya kusitisha mapigano na Israel yamefifia.

https://p.dw.com/p/4cd7j
Qatar Doha | Mkuu wa Hamas Ismail Haniyya
Ismail Haniyeanakutana na maafisa wa Misri kujadili hali ya kisasa na mazingira ya ndani ya Gaza.Picha: Iranian Foreign Ministry/ZUMA Wire/IMAGO

Taarifa ya Hamas imesema Haniyeh, kiongozi wa ofisi ya kisiasa ya kundi hilo la Kipalestina yenye makao yake nchini Qatar, atafanya mazungumzo na maafisa wa Misri kuhusu hali ya kisiasa na mazingira ya Gaza.

Ujumbe wa Haniyeh pia utajadili juhudi za kukomesha uvamizi, kutoa misaada kwa raia na kufanikisha malengo ya watu wa Palestina, imeongeza taarifa hiyo.

Licha ya mkururo wa mikutano na wapatanishi wa Israel na Hamas wiki iliyopita, wapatanishi wa Misri, Qatar na Marekani hawakupata muafaka katika juhudi zao za kupumzisha mapigano yaliodumu kwa zaidi ya miezi minne.

Waziri Mkuu wa Qatar alionesha mashaka hayo wakati wa mkutano wa kimataifa wa usalama wa Munich siku ya Jumamosi.

Katika taarifa siku ya Jumamosi, Haniyeh alirudia matakwa ya Hamas, licha ya baadhi ya matakwa hayo kutupiliwa mbali na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliyeyafananisha na njozi.

Soma pia: Israel yaitwanga Gaza kabla ya kura ya usitishaji vita UM

Matakwa hayo yanahusisha usitishaji vita, uondoaji wa vikosi vya Israel Gaza, kukomesha mzingiro wa ukanda huo na hifadhi salama kwa mamia ya maelfu ya raia wa Kipalestina waliohama makaazi yao.

Israel imeapa kuiangamiza Hamas kulipiza shambulio lake lisilo kifani la Oktoba 7, lililosababisha vifo vya watu 1,160, wengi wao raia kulingana na takwimu za Israel.

Deutschland | MMkutano wa Usalama wa Munich | Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani, Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar
Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani alisema matumaini ya muafaka kati ya pande mbili yalififia.Picha: Tobias Koehler/MSC

Mashambulizi yake ya kujibu yameua takribani Wapalestina elfu 30 kufikia sasa huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kwa mujibu wa wizara ya afya ya ukanda huo inayosimamiwa na Hamas.

Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, limesema moja kati ya watoto sita katika eneo lililotelekezwa la Gaza Kaskazini, wanakabiliwa na utapiamlo mbaya, huku Israel ikiapa kutanua mashambulizi yake dhidi ya Hamas katika mji wa kusini zaidi wa Rafah.

Mkuu wa jumuiya ya mataifa ya Kiarabu Ahmed Aboul Gheit, ameitolea wito jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za mara moja kuzuwia operesheni ya Israel Rafah.

"Nakariri msimamo wetu wa wazi wa kukataa vitisho vya Israel vya kuuvamia mji wa Rafah, ambao umekuwa kimbilio la mwisho kwa Wapalestina zaidi ya milioni moja na nusu waliokimbia uvamizi na uharibifu katika maeneo mengine ya Ukanda huo," alisema Aboul Gheit.

"Na tena, natoa wito kwa pande zote kuchukua hatua madhubuti kuzuwia operesheni hii ya kikatili ambayo inaweza kuwa na matokeo mabaya kwa usalama wa kikanda," aliongeza.

Marekani yapiga kura ya turufu ya tatu dhidi ya hatua za Umoja wa Mataifa

Marekani ilipinga azimio la Umoja wa Mataifa linaloungwa mkono na Waarabu Jumanne kutaka kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa sababu za kibinadamu katika vita vya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.

Kura katika Baraza la Usalama lenye wanachama 15 kura hiyo iliungwa mkonoa na wanachama 13-1 huku Uingereza ikijizuwia, jambo linaloonyesha uungaji mkono mkubwa wa kimataifa wa kumaliza vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya miezi minne.

Soma pia: Israel yatishia kushambulia Rafah wakati wa Ramadhan

Ilikuwa kura ya tatu ya turufu ya Marekani juu ya azimio la Baraza la Usalama la kutaka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.

"Kuendelea na upigaji kura leo ilikuwa ni ndoto za mchana na kutowajibika... hatuwezi kuunga mkono azimio ambalo lingeweka mazungumzo nyeti hatarini," alisema balozi wa Washington katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield wakati akitetea azimio mbadala lililoandaliwa na Marekani.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa | Mkutano wa kupigia kura azimio la kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield akiinua mkono wake kupiga kura ya pekee na ya turufu dhidi ya azimio la kusitisha vita kati ya Israel na HamasPicha: Seth Wenig/AP Photo/picture alliance

"Kudai kusitishwa kwa mapigano mara moja na bila masharti bila makubaliano yanayohitaji Hamas kuwaachilia mateka hakutaleta amani ya kudumu. Badala yake, kunaweza kuendeleza mapigano kati ya Hamas na Israel," alisema.

Marekani imependekeza rasimu ya azimio linalotaka kusitishwa kwa muda kwa vita vya Israel na Hamas na kupinga mashambulizi makubwa ya ardhini ya mshirika wake Israel huko Rafah, kwa mujibu wa maandishi yaliyoonekana na Reuters. Ilisema inapanga kuruhusu muda wa mazungumzo na haitaharakisha kupiga kura.

Hadi sasa, Washington imekuwa ikichukia neno kusitisha mapigano katika hatua zozote za Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya Israel na Hamas, lakini maandishi ya Marekani yanaangazia lugha ambayo Rais Joe Biden alisema aliitumia wiki iliyopita katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Rasimu ya azimio la Marekani inatazamia Baraza la Usalama "kutilia mkazo uungaji mkono wake kwa usitishaji mapigano kwa muda Gaza haraka iwezekanavyo, kwa kuzingatia fomula ya mateka wote kuachiliwa, na kutoa wito wa kuondoa vizuizi vyote vya utoaji wa msaada wa kibinadamu kwa kiwango kikubwa."

Azimio lililoandaliwa na Algeria lililopigiwa kura ya turufu na Marekani halikuhusisha kusitishwa kwa mapigano na kuachiliwa kwa mateka. Badala yake lilidai kando usitishaji mapigano wa haraka wa kibinadamu na kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote.

Afrika Kusini yaiambia ICJ kwamba inaishutumu Israel kwa ubaguzi dhidi ya Wapalestina

Huko mjini The Hague, wawakilishi wa Afrika Kusini wamehoji kuwa Israel inahusika na ubaguzi wa rangi na utengano dhidi ya Wapalestina, na kwamba ukaliaji wa Israel wa ardhi inayotafutwa na Wapalestina kwa ajili ya taifa lao la baadae ni ukiukaji wa kimsinga wa sheria ya kimataifa. Israel inapinga madai hayo.

Wawakilishi hao wa Afrika Kusini walikuwa wakizungumza katika siku ya pili ya vikao vya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ, kuhusu ombi la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuitaka itoa maoni ya ushauri usiofungamana na sheria kuhusu uhalali wa sera za Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.

Uholanzi The Hague | Mahakama ya Kimataifa ya Haki | Kesi ya mauaji ya kimbari ya Israel | Tangazo kuhusu maombi ya dharura
Afrika Kusini imehoji katika mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa ICJ, kwamba Israel inahusika na ubaguzi wa rangi na utengano dhidi ya Wapalestina, na kwamba ukaliaji wake wa maeneo ya Wapalestina unakiuka sheria ya kimataifa.Picha: Piroschka van de Wouw/REUTERS

"Afrika Kusini ina wajibu maalum, kwa watu wake na jumuiya ya kimataifa, kuhakikisha kwamba popote pale ambapo vitendo viovu na vya kuudhi vya ubaguzi wa rangi vinapotokea, ni lazima vitajwe kwa jinsi vilivyo na kukomeshwa mara moja," balozi wa Afrika Kusini nchini Uholanzi, Vusimuzi Madonsela, aliliambia jopo la majaji 15 wa kimataifa.

Israel inakanusha shutuma za ubaguzi wa rangi na kwa kawaida inayakosoa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mahakama za kimataifa kuwa hazitowi haki na zenye upendeleo dhidi yake. Israel haitoi tamko wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, ambayo inafanyika katikati mwa vita vya Gaza ambavyo vimeua zaidi ya Wapalestina 29,000, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza.

Soma pia: Waziri wa Wapalestina aishutumu Israel kwa ubaguzi wa rangi

Israel ilituma utetezi wake wa maandishi mwaka jana ambamo ilisema kwamba maswali yaliyowasilishwa mahakamani ni ya upendeleo na "yanashindwa kutambua haki na wajibu wa Israel kulinda raia wake," kushughulikia masuala ya usalama wa Israel au kukubali makubaliano ya awali na Wapalestina ya kujadili "hadhi ya kudumu ya eneo hilo, mipangilio ya kiusalama, makazi na mipaka."

Israel iliuteka Ukingo wa Magharibi, Jerusalem mashariki na Ukanda wa Gaza katika vita vya 1967 vya Mashariki ya Kati. Wapalestina wanayataka maeneo yote matatu kwa ajili ya taifa lao huru. Israel inauchukulia Ukingo wa Magharibi kuwa eneo linalozozaniwa na inasema mustakabali wake unapaswa kuamuliwa katika mazungumzo.

Israel pia imejenga makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi, ambayo mengi yanafanana na vitongoji na miji midogo iliyoendelea kikamilifu. Makaazi hayo yanakaliwa na walowezi wa Kiyahudi zaidi ya 500,000, huku Wapalestina wapatao milioni 3 wakiishi katika eneo hilo. Israel iliiteka Jerusalem ya mashariki na inauchukulia mji mzima kuwa mji mkuu wake.

Kwanini Afrika Kusini inaishtaki Israel ICJ?

Jumuiya ya kimataifa inachukulia kwa kiasi kikubwa makazi hayo kuwa haramu. Unyakuzi wa Israel wa Jerusalem mashariki, nyumbani kwa maeneo matakatifu sana ya jiji hilo, hautambuliki kimataifa.

Soma pia: Israel yakabiliwa na shinikizo jipya kutoka Marekani dhidi ya kuishambulia Rafah

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema katika taarifa yake Jumatatu kwamba Israel haitambui uhalali wa majadiliano katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki. Aliitaja kesi hiyo kuwa "sehemu ya jaribio la Wapalestina la kulazimisha matokeo ya makubaliano ya kisiasa bila mazungumzo."

Mwakilishi wa Afrika Kusini Pieter Andreas Stemmet aliiambia mahakama siku ya Jumanne kwamba makazi hayo yamepanua "hali ya muda ya uvkaliaji huo na kuwa hali ya kudumu inayokiuka haki ya Wapalestina ya kujitawala."

Hoja za kisheria za Afrika Kusini ziliakisi zile zilizotolewa siku moja mapema na wawakilishi wa Palestina katika ufunguzi wa siku sita za usikilizaji wa kesi hiyo mbele ya mahakama hiyo yenye makao yake makuu Uholanzi. Baada ya Wapalestina kufungua kesi hiyo, jumla ya mataifa 51 na mashirika matatu ya kimataifa yamepangwa kuihutubia mahakama hiyo, ambayo huenda ikachukua miezi kadhaa kutoa maoni yake ya ushauri.

Chanzo: Mashirika