1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Kenya yasema kikosi chake kitapelekwa Haiti hivi karibuni

19 Mei 2024

Kenya imesema leo kikosi cha polisi wa nchi hiyo kitapelekwa Haiti ndani ya wiki chache zinazokuja kuongoza ujumbe wa kimataifa wa kusaidia kupambana na magenge ya wahalifu.

https://p.dw.com/p/4g3KS
Machafuko Haiti
Machafuko yatokanayo na makundi ya wahalifu nchini Haiti. Picha: Guerinault Louis/Anadolu/picture alliance

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Kenya, Korir Sing´Oei. Alikuwa akizungumza na waandishi habari muda mfupi kabla ya Rais William Ruto kuanza safari ya kwenda Marekani kwa mkutano na Rais Joe Biden mnamo Mei 23.

Kenya iliahidi Julai mwaka jana kupeleka kikosi cha askari 1,000 nchini Haiti kulisaidia taifa hilo la kanda ya Karibia kurejesha utulivu baada ya kuandamwa na kiwingu cha ghasia za makundi ya wahalifu.

Hata hivyo mpango huo wa Kenya umekumbwa na misukosuko kufuatia kufunguliwa kwa kesi kadhaa za kuupinga. Hapo kabla mahakama moja nchini humo ilisema mpango huo ni kinyume na katiba na kwamba haupaswi kutekelezwa hadi pale Kenya na Haiti zitakapofikia mkataba wa pamoja wa usalama.

Serikali iliharakisha kupatikana mkataba huo uliosainiwa mnamo Machi 1.