1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Sudan lakataa kusitisha mapigano mwezi wa Ramadhani

Bruce Amani
11 Machi 2024

Jeshi la Sudan limesema hakutakuwa na makubaliano ya usitishaji mapigano wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani hadi pale wanamgambo wa RSF watakapoondoka kwenye makaazi na maeneo ya raia.

https://p.dw.com/p/4dNpT
Sudan Khartoum Abdel Fattah al-Burhan
Mkuu wa Jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ameukataa wito wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha mapigano kuupisha mwezi mtukufu wa Ramadhani.Picha: ASHRAF SHAZLY/AFP/Getty Images

Afisa wa ngazi za juu wa vikosi vya jeshi la Sudan, Jenerali Yasser al-Atta, amesema hayo katika taarifa kupitia mtandao wa Telegram, baada ya wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa usitishwaji wa mapigano wakati wa Ramadhani, ambao ulikuwa umepokelewa vyema na wanamgambo wa RSF.

Soma zaidi: Mazungumzo ya kutafuta amani ya Sudan yakwama Jeddah

Taarifa ya Atta iliyoangazia hatua za hivi karibuni za jeshi katika mji wa Omdurman, unaochukua sehemu kubwa ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum, imesisitiza kwamba hawatasitisha mapigano hadi RSF watakapotimiza ahadi waliyoitoa Mei mwaka uliopita wakati wa mazungumzo yaliyosimamiwa na Saudi Arabia na Marekani mjini Jeddah ya kuondoka kwenye maeneo hayo.