1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaThailand

Indonesia yahimiza suluhisho la kisiasa Myanmar

12 Julai 2023

Indonesia ambayo ndiyo mwenyekiti wa sasa jumuiya ya mataifa ya ASEAN, imehimiza suluhisho la kisiasa nchini Myanmar ambako mjumbe wa Thailand alitangaza alikutana na aliekuwa kiongozi wa kidemokrasia Aung San Suu Kyi.

https://p.dw.com/p/4TmlK
Indonesien | ASEAN Gipfel 2023 in Jakarta
Picha: Achmad Ibrahim/AP Photo/picture alliance

 Myanmar imekumbwa na ghasia mbaya tangu mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Suu Kyi zaidi ya miaka miwili iliyopita, na kusababisha ukandamizaji wa umwagaji damu dhidi ya wapinzani.

Jumuiya hiyo ya mataifa 10 wanachama ya Kusini Mashariki mwa Asia kwa muda mrefu imekuwa ikitajwa kama chombo cha maongezi tu kisicho na meno.

Inatazamwa kugawanyika juu ya juhudi za kidiplomasia za kutatua mgogoro huo, wakati ikijaribu kuunda msimamo wa pamoja kuhusu Myanmar, taifa linalotawaliwa na jeshi. 

Waziri wa mambo ya nje wa Indonesia Retno Marsud, amewambia wanzake wa ASEAN katika hotuba yake ya ufunguzi wa siku ya pili ya mazungumzo mjini Jakarta, kwamba suluhisho la kisiasa pekee ndiyo litaleta amani ya kudumu.

Soma pia:UN: Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutafakari mwelekeo wake katika mgogoro wa Myanamar
Amesema mazungumzo yatafungua njia kwa suluhisho la kisiasa. Ni suluhisho la kisiasa pekee ndiyo litaleta amani ya kudumu.

"Bado tuna wasiwasi mkubwa kuona ghasia zinazoendelea na kuongezeka kwa vurugu nchini Myanmar." Alisema

Aliongeza kwamba "Indonesia inalaani vikali matumizi ya nguvu na ghasia."

Mwanadiplomasia huyo amesema taifa lake linahimiza wadau wote kukemea vurugu kwani hili ni jambo la msingi kujenga imani.

Mkutano washwangazwa na mjumbe wa Thailand

Mkutano huo ulipatwa na mshangao wakati waziri wa mambo ya nje wa Thailand alipofichua kwamba alikutana kivyake na kiongozi wa kidemokrasia wa Myanmar aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyisiku ya Jumapili katika mji mkuu wa nchi hiyo Naypyidaw, na kusema alikuwa  na afya njema.

Waziri huyo Don Pramudwini amewaambia waandishi habari kandoni mwa mkutano wa mawaziri kwamba katika mkutano wake na Suu Kyi ambaye ameonekana mara moja tu tangu azuiliwe baada ya mapinduzi mapema 2021, mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel alihimiza mazungumzo.

UN: Mauaji bado yanaendelea Myanmar

Waziri wa mambo ya nje wa Ufilipino amesema Don aliwaarifu mawaziri wa ASEAN kuhusu mkutano wake wa Suu Kyi.

Soma pia:Jeshi Myanmar lampinga ujumbe wa ASEAN

Amesisitiza kuwa juhudi zozote huru za kuanzisha tena machakato wa amanizinapaswa kuwiana na mpango wa nukta tano wa ASEAN uliokubaliwa miaka miwili iliyopita na utawala wa kijeshi wa Myanmar.

Mwanadiplomasia mkuu wa Indonesia amerudia msimamo wa kanda hiyo kwamba kuanzishwa tena kwa mazungumzo kati ya pande zinazozozana za Myanmar na mapatano ya kisiasa yaliyojadiliwa ndiyo njia pekee ya kumaliza machafuko yaliodumu kwa zaidi ya miaka miwili.

Juhudi za ASEAN kuanzisha mpango wa mambo matano unaotaka kukomeshwa kwa ghasia na mazungumzo mapya ya amani hazijazaa matunda.

Huku serikali ya Myanmar ikipuuza ukosoaji wa kimataifana kukataa kushirikiana na wapinzani wake. Juhudi za kanda hiyo zinakwamishwa na kanuni za mkataba wake wa maafikiano na kutoingilia kati.

Mawaziri walikuwa wanajaribu kukubaliana juu ya msimamo wa pamoja kuhusu Myanmar katika siku ya pili ya mazungumzo lakini mwanadiplomasia moja wa kanda hiyo amesema tamko litatolewa mwishoni mwa mkutano huo kesho Jumatano.