1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ataka usitishaji mapigano Gaza, Sudan

Bruce Amani
11 Machi 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametoa wito wa kuwekwa chini silaha katika vita vya Israel huko Ukanda wa Gaza na pia kwenye mzozo nchini Sudan wakati mwezi mtukufu wa Kiislamu wa Ramadhani ukianza.

https://p.dw.com/p/4dOim
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametaka vita visitishwe kwenye Ukanda wa Gaza na pia nchini Sudan katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.Picha: Karim Jaafar/AFP/Getty Images

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alitoa pia wito wa kuachiwa mateka wanaoshikiliwa na kundi la Hamas na kuondolewa kwa vizingiti vyote ili kuhakikisha upelekaji wa misaada ya dharura katika kasi na kiwango kikubwa kinachohitajika Gaza.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa wahofia mzozo wa Sudan kuongeza wakimbizi

Umoja wa Mataifa unaonya kuwa robo ya wakaazi wako ukingoni mwa kukabiliwa na njaa. 

Wakati hayo yakijiri, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallan amesema mamlaka nchini humo zitaheshimu uhuru wa kuabudu wakati wa mfungo wa Ramadhani, lakini ziko "tayari" kwa mtu yeyote atakayevuruga amani.

Soma zaidi: Ramadhani yaanza bila usitishwaji vita Gaza

Kauli ya Yoav inatolewa wakati kukiwa na wasiwasi wa kutokea ghasia kipindi hiki cha Ramadhani katika Msikiti wa Al-Aqsa baina ya waumini wa Kiislamu na mamlaka za Israel.

Wapatanishi wa mzozo huo walitumai kupata muafaka wa kusitishwa mapigano kabla ya kuanza kwa kipindi hiki cha Ramadhani, lakini mpaka sasa hakuna mafanikio.