1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Greta Thunberg akamatwa, ashitakiwa London

Josephat Charo
18 Oktoba 2023

Mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg ameshitakiwa kwa kosa la kuvuruga utaratibu wa umma baada ya kukamatwa kwenye maandamano dhidi ya mkutano wa sekta ya mafuta na gesi jijini London.

https://p.dw.com/p/4XhNX
UK Protest Klimaaktivistin Greta Thunberg
Mwanaharakati wa mazingira, Greta Thunberg (wa pili kulia), akitiwa nguvuni na polisi ya London.Picha: Kin Cheung/AP/picture alliance

Polisi ya London imesema mwanaharakati huyo wa umri wa miaka 20 raia wa Sweden alikuwa miongoni mwa watu 26 walioshitakiwa baada ya waandamanaji kukusanyika nje ya hoteli ya kifahari ya Intercontinental wakati wa mkutano kuhusu nishati.

Wanaharakati hao walipia makelele wakipinga fedha zinazotokana na mafuta na kujaribu kuwazuia wajumbe wasiingie katika hoteli hiyo siku ya Jumanne (Oktoba 17).

Soma zaidi: Wanaharakati wa mazingira kuendeleza maandamano leo

Polisi wamesema Thunberg alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi kabla kuachiliwa kwa dhamana mpaka Novemba 15 wakati kesi yake itakaposikilizwa katika mahakama ya Westminster jijini London.