1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

England wawachaza Ireland Kaskazini 5-0 mechi ya mwisho

Iddi Ssessanga
16 Julai 2022

England imeigaragza jirani yake Ireland Kaskazini kwa kuipiga mabao 5-0 kwenye mechi ya mwisho ya awamu ya makundi na kujihakikishia ushindi wa kishindo kuelekea robo fainali ya michuano ya soka ya wanawake barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/4EE3U
Frauen Fußball EM 2022 | Nordirland - England
Picha: Harriet Lander/Getty Images

Wenyeji England wameendelea kukanyaga mafuta kwenye michuano ya Euro ya Wanawake kwa kuilaza Ireland ya Kaskazini mabao 5-0 katika mechi ya mwisho ya kundi A siku ya Ijumaa, licha ya kuwa tayari wamefuzu hatua ya robo fainali wakiwa usukani mwa kundi lao.

Kikosi hicho cha Sarina Wiegman kilikuwa kimejihakikishia nafasi ya kucheza nane bora kwa ushindi wa 8-0 dhidi ya Norway siku ya Jumatatu lakini wakaendeleza kasi hiyo katika mechi yao kwenye Uwanja wa St Mary's dhidi ya wapinzani kutoka ng'ambo ya bahari ya Ireland.

Soma pia: Ufaransa yatinga robo fainali baada ya kuipiga Ubelgiji 2-1

Mshambulizi wa Chelsea, Fran Kirby alifungua karamu ya mabao kwa shuti kali dakika ya 40 kabla ya Beth Mead kunyakua bao lake la tano kwenye michuano hiyo muda mfupi baadae na kumpeleka nafasi ya kwanza kwenye orodha ya wafungaji.

Frauen Fußball EM 2022 | Nordirland - England
Wachezaji wa timu ya wanawake ya England wakisherehekea moja ya mabao yao dhidi ya Ireland Kaskazini, mjini Southampton, Julai 15, 2022.Picha: Lisi Niesner/REUTERS

Ireland Kaskazini, ambayo ndiyo timu inayoshika mkia kiviwango kwenye michuano ya Euro, ilifanya kila iwezalo kuzuia wimbi la Uingereza lakini shuti kali la haraka kutoka kwa Alessia Russo muda mfupi baada ya kipindi cha mapumziko liliharibu matumaini waliyokuwa nayo ya kubakisha mabao chini.

Jioni ilizidi kuwa mbaya kwa kikosi cha Kenny Shiels baada ya jaribio la kuondosha shuti la Kelsie Burrows dakika ya 75 kumpita kipa Jacqueline Burns na kutinga wavuni mwake na kufanya mabao kuwa 5-0 kwa England.

Austria yaiondoa Norway, yaweka miadi na Ujerumani robo fainali

Katika mechi nyingine iliyochezwa jana usiku, Norway ilitolewa kwa mshtuko kwenye michuano hiyo baada ya washindani hao wa taji kabla ya kinyang'anyiro kuambulia kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Austria.

Soma pia: Euro 2022: Timu ya wanawake ya Ujerumani yaiadhibu Uhispania 2-0 na kutinga robo fainali

Licha ya kuwepo kwa nyota wa Lyon Ada Hegerberg katika kikosi chao, mabingwa wa zamani wa Ulaya Norway walilipa gharama kwa kuonyesha mchezo mwingine usiovutia mjini Brighton.

Norway ilishindwa kusonga mbele kutoka Kundi A baada ya kushindwa kwa mara ya pili mfululizo, huku Austria ikifuzu kucheza robo fainali kama washindi wa pili nyuma ya England.

Frauen Fußball EM 2022 | Österreich - Norwegen
Wachezaji wa Austria wakishangilia bao lao la pekee dhidi ya Norway mjini Brighton, England, Julai 15, 2022.Picha: Pedro Soares/SheKicks/SPP/IMAGO

Wakihitaji ushindi ili kwedna juu ya Austria katika mechi yao ya mwisho ya kundi, Norway walianza kuonyeshwa mlango wa kuaga michuano hiyo baada ya dakika 37 wakati Nicole Billa alipofunga kwa kichwa krosi ya Verena Hanshaw.

Wanorway hawakuweza kurejea na ni Austria ambao wangeweza kushinda kwa tofauti kubwa kutokana na umaliziaji bora.

Kipa wa Norway Guro Pettersen aliokoa mara kadhaa ili kuipa timu yake nafasi, lakini Manuela Zinsberger wa Austria aliwazuia Celin Bizet na Hegerberg katika hatua za mwisho.

Wakicharazwa 8-0 na England katika mchezo wao wa awali, michuano ya Norway iligeuka kuwa shubiri baada ya matumaini ya awali yaliyochochewa na ushindi wa 4-1 dhidi ya Ireland Kaskazini katika mechi yao ya kwanza ya kundi.

Huku Norway ikirejea nyumbani, Austria wanatazamia kucheza na mabingwa mara nane wa Ulaya, Ujerumani, katika robo-fainali mjini Brentford siku ya Alhamisi.

Chanzo: Mashirika